NEWS

Sunday, 27 July 2025

Wajumbe kura za maoni CCM wanoa ‘vichinjio’ wakisubiri mkeka wa watia nia ubunge, udiwani watakaopenya vikao vya juu



Na Mwandishi Wetu

Kesho Jumatatu ya Julai 28, 2025 ni siku ya kipekee iliyobeba ndoto za watia nia wa nafasi za ubunge na udiwani kote nchini, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajiwa kuanza kuweka hadharani orodha ya majina ya waliopenya hatua ya kwanza ya mchujo na kurejeshwa majimboni kwa ajili ya kuchuana kwenye kura za maoni.

Joto la kisiasa ni kali - na bila shaka katika kila kona ya nchi gumzo ni moja tu: “Nani karudi? Nani kakatwa?” Wajumbe wa kura za maoni majimboni nao wamejaa hamasa, wakiwa wamejiandaa kufanya maamuzi magumu.

Ni siku ya hofu kwa baadhi, siku ya ushindi wa awali kwa wengine, na kwa CCM ni siku ya kuonesha umakini wake katika kuleta timu ya watia nia imara, ambao baadaye miongoni mwao watateuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho tawala katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Inaelezwa kuwa vikao vya maamuzi vya CCM ngazi ya taifa vinavyoendelea jijini Dodoma vinapitia kwa kina na umakini mkubwa majina ya watia nia, huku vigezo vya uadilifu, rekodi ya utendaji na uwezo wa kuunganisha jamii vikizingatiwa.

Kwa ujumla, wanachama wa CCM na Watanzania kwa ujumla wameelekeza macho na masikio yao Dodoma wakisubiri kwa shauku kubwa majina yaliyochomoza - mithili ya wanafunzi wanaosubiri matokeo ya mtihani wa kitaifa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages