
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo elekezi kwa wafanyakazi wapya wa shirika hilo jijini Dodoma juzi.
------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) wamehimizwa kufanya kazi kwa uadilifu ili liendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema mwenendo mwema wa wafanyakazi kuhusu suala la uadilifu ni kichocheo cha ufanisi bora wa chombo hicho cha umma.
Dkt. Nyansaho aliyasema hayo jijini Dodoma juzi, wakati wa uzinduzi wa mafunzo elekezi kwa wafanyakazi wapya wa shirika hilo.
Aliwataka wafanyakazi hao kutambua uzito wa fursa ya utumishi waliyoipata kwa kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na juhudi kubwa ili TANESCO iwe kielelezo cha utendaji bora wa kazi katika taasisi za umma.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia kibali cha kuajiri. Hii ni fursa ya kipekee na ni wajibu wenu kuithamini kwa kufanya kazi kwa juhudi na weledi mkubwa,” Dkt. Nyansaho alisema.
Aliwakumbusha kuwa TANESCO imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma bora kwa wateja wake, hivyo ni bora kazi hiyo ikaendelezwa kwa kuzingatia nidhamu, uadilifu na utendeji uliotukuka.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, aliwataka wafanyakazi wapya kuwa mabalozi katika maeneo yao ya kazi kwa kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa wateja.
“Mnakwenda kukutana na wateja wetu. Wahudumieni kwa heshima na moyo wa kujitolea ili kwa pamoja tuendelee kujenga taswira chanya ya TANESCO,” Twange alisema.
Hivi karibuni, TANESCO iliajiri wafanyakazi 555 kupitia michakato mbalimbali.
Unaweza pia kusoma:
»MAKALA YA MAJI:Mradi wa bilioni 21/- kuboresha huduma ya maji mjini Mugumu, RC Mara amtaka mkandarasi kuukamilisha kwa wakati
»MAKALA YA SIASA:Janeth Mtiba: Kada wa CCM mwenye umri mdogo zaidi aliyetia nia ubunge jimbo la Tarime Mjini
»UTALII WA NDANI:RC Mara awakaribisha waandishi kutembelea Hifadhi ya Serengeti, kugonga kichuri
No comments:
Post a Comment