
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyayo Tanzania, Mary Joseph Daniel (kulia), Kaimu DED Serengeti, Victor Rutonesha (aliyevaa koti jeusi) na baadhi ya viongozi wengine na wanafunzi wakati wa hafla ya uzinduzi wa mashindano ya SAMIA UWEZO AWARD 2025 mjini Mugumu, Serengeti jana.
--------------------------------------------
Katika jitihada za kujenga kizazi cha vijana wenye uelewa, uwezo na moyo wa kujitolea kwa jamii zao na taifa kwa ujumla, Shirika la Nyayo Tanzania kwa kushirikiana na Great Hope Foundation wamezindua rasmi mashindano ya SAMIA UWEZO AWARD Mkoa wa Mara 2025, wakianza na wilaya za Tarime na Serengeti.
Great Hope Foundation imekua ikifanya mradi wa UWEZO AWARD kwa mwaka wa 10 sasa katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani, ambapo imejizolea sifa kama jukwaa bora la kuibua vipaji, kukuza ujasiriamali na kuandaa viongozi wa kesho wakiwa bado shuleni.
Uzinduzi wa SAMIA UWEZO AWARD 2025 ulifanyika jana Julai 18, 2025 mjini Mugumu, Serengeti na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Wilaya, maafisa elimu na maendeleo ya jamii, wakuu wa shule, walimu na wanafunzi wa shule za sekondari kutoka wilaya za Tarime na Serengeti.


Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyayo Tanzania, Mary Joseph Daniel, mashindano hayo yanalenga kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa vitendo - kwa kuhakikisha wanafunzi wanajifunza si tu kwa nadharia, bali pia kwa vitendo.
“Kwa kutambua jitihada kubwa na dira ya maendeleo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuinua ubora wa elimu kupitia Competence-Based Curriculum (CBC), Shirika la Nyayo Tanzania liliamua kuyapa mashindano haya jina lake kwa heshima.
Mary akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mashindano ya SAMIA UWEZO AWARD 2025 mjini Mugumu, Serengeti jana Julai 18, 2025.
-----------------------------------------
Mary alisema mashindano ya SAMIA UWEZO AWARD Mkoa wa Mara 2025 yatashirikisha shule za sekondari 30 kutoka wilaya za Tarime na Serengeti, ambapo wanafunzi watashindana kufanya miradi ya kijasiriamali itakayoleta mabadiliko chanya katika jamii.
Mashindano hayo ni ushahidi mwingine kuwa uwekezaji katika elimu ya vitendo kwa vijana ni unasaidia kujenga Tanzania yenye vijana wabunifu, jasiri na wanaojali jamii na taifa lao kwa maendeleo endelevu.

Mary alifafanua kuwa mashindano ya SAMIA UWEZO AWARD 2025 yatahusisha ushindani wa vipaji maalum, ubunifu wa miradi ya ujasiriamali na mawazo yanayosaidia kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Alitaja zawadi zitakazotolewa kuwa ni na tuzo kwa washiriki, shilingi milioni moja kwa mshindi wa kwanza, silingi laki tano kwa mshindi wa pili na shilingi laki tatu kwa mshindi wa tatu.
No comments:
Post a Comment