NEWS

Monday, 7 July 2025

Mfahamu Nicolaus Mgaya “Chichake” mtia nia ya ubunge Tarime Vijijini



Nicolaus Mahando Mgaya “Chichake”

Na Mwandishi Maalumu

Wiki iliyopita, wakati jua likielekea kuchwea katika viunga vya Nyamongo, tulikutana na kijana mwenye uso wa matumaini, macho ya uthubutu na kauli ya kuhamasisha. Huyu si mwingine, bali ni Nicolaus Mahando Mgaya - maarufu kwa jina la Chichake, jina linalozidi kushika kasi katika jimbo la Tarime Vijijini kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa maneno mengine, tunaweza kusema Chichake ambaye tayari ni mtia nia ya ubunge Tarime Vijijini, ni nyota mpya ya matumaini chanya kwa wananchi wa jimbo hilo.

Mazungumzo yetu yanaanza kwa furaha, na bila kuchelewa Chichake anaanza kueleza kwa kifupi kilichomsukuma kuingia kwenye siasa, na hasa kutia nia ya ubunge wa Tarime Vijijini.

Anasema kwanza kabisa, ni mapenzi makubwa aliyonayo kwa wananchi wa Tarime Vijijini. “Nimezaliwa hapa, nimekulia hapa, nimeona na kuishi changamoto zao,” anasema.

Anaendelea: “Ninaamini jimbo letu lina kila sababu ya kuwa mfano wa maendeleo kwa nchi nzima kwani tuna ardhi nzuri, watu wachapa kazi na rasilimali nyingi, lakini bado tupo nyuma. Nimeamua kugombea kwa sababu naamini mabadiliko tunayoyataka yanaanza na sisi vijana kuamua kusimama na kuwajibika.”

Chichake anasema dira yake ni Tarime Vijijini yenye huduma bora za afya, elimu, maji safi, barabara zinazopitika, ajira kwa vijana na maendeleo ya kweli ya kiuchumi kwa wananchi wote.

Aidha, anataka kuona wakulima wakipata masoko ya uhakika, wachimbaji wadogo wakiwezeshwa na kupewa heshima, na wanawake wakishiriki kikamilifu katika mnyororo wa uchumi.

Katika zama hizi ambazo taifa linahitaji viongozi wenye maono mapana, dhamira thabiti na moyo wa kweli wa kuwatumikia wananchi kwa tija, Chichake ni miongoni mwa watia nia wachache wanaotajwa kuwa na sifa za kuongoza kwa mafanikio jimbo la Tarime Vijijini.

Ni kijana msomi, mwadilifu, mzalendo na mbunifu anayejipambanua kuwa na maono ya kuleta mageuzi makubwa ya kuinua makundi yote ya wananchi wa Tarime Vijijini kiuchumi na kijamii.

Ni kada kijana wa Chama Cha Mapunduzi (CCM) mwenye maarifa, mchapakazi, mzalendo wa kweli na mwenye uwezo wa kuwakilisha sauti za wananchi wa kawaida ambao kwa muda mrefu wametamani maendeleo yanayogusa maisha yao moja kwa moja.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2025 ni fursa muhimu kwa wananchi wa jimbo la Tarime Vijijini kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wa maendeleo yao.

Tayari Chichake ametangaza kuingia kwa kishindo kwenye kinyang’anyiro cha kuomba uteuzi wa kugombea nafasi ya ubunge, - akiwa na ndoto ya kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii katika jimbo la Tarime Vijijini.

Ni kijana aliyekulia kwenye changamoto zinazowakabili watu wa Tarime Vijijini. Kwa ubunifu, ujasiri, upendo na moyo wa kujitolea, anakuja na ajenda mpya ya kuunganisha nguvu za wananchi na rasilimali za eneo lao kwa ustawi wa wote.

Kwa mtazamo wake, hali halisi ya sasa ya maisha ya wakazi wa jimbo hilo haiakisi neema ya utajiri wa rasilimali na fursa lukuki za kiuchimi zilizopo.

“Jimbo la Tarime Vijijini ni tajiri lakini jamii yetu ni maskini, fursa zilizopo haziwanufaishi wananchi,” anasema Chichake.

Anasema jimbo hilo linahitaji kiongozi makini na mwenye uwezo wa kulibadilisha lifanane na hadhi ya utajiri wa rasilimali zilizopo, ikiwa ni pamoja na madini aina ya dhahabu.

“Ninatamani kuona vijana katika jimbo hili wanajengewa uwezo wa kujiajiri na kuajiri wengine, lakini pia wanapewa elimu ya kupata mikopo inayotolewa na halmashauri ili waweze kujikomboa kiuchumi,” anasema Chichake.

Anasisitiza pia umuhimu wa siasa za staha kipindi hiki cha kuelekea kwenye michakato ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika nchini Oktoba 2025.

“Tufanye siasa za kistaarabu, tuwe na umoja na kumtanguliza Mungu ili tuweze kufanya maamuzi sahihi yatakayosaidia jamii yetu kuondokana na umaskini,” anasema Chichake.

Kuzaliwa, malezi na elimu
Nicolaus Mahando Mgaya “Chichake” alizaliwa Juni 18, 1983 katika kijiji cha Nyamongo, wilaya ya Tarime mkoani Mara. Alilelewa na kupata elimu katika mazingira yanayomfanya kuelewa kwa undani changamoto halisi na matarajio ya watu wa Tarime Vijijini.

Anasema alihitimu elimu ya msingi mwaka 1998 katika Shule ya Msingi Nyamongo na mwaka 2002 alihitimu elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Nyamongo.

Mwaka 2008 alihitimu Astashahada ya Uhasibu katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam, mwaka 2010 alihitimu Stashahada (Diploma) ya Mauzo na Masoko na mwaka 2011 alihitimu Shahada (Digrii) ya Kwanza ya Uhasibu huko huko IFM Dar es Salaam.

Aidha, Chichake anasema amepata kozi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu ya ujasiriamali, lakini pia mafunzo ya vitendo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Dar es Salaam.

Akiwa na elimu ya juu na mafunzo ya kitaaluma yanayomuwezesha kusimamia maendeleo kwa weledi, Chichake ni mzalendo wa kweli mwenye maono mapana ya kuleta ustawi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa wananchi wote - bila kujali tofauti zao.

Kama kijana aliyelelewa katika misingi ya maadili ya Kitanzania, anasifika kwa unyenyekevu, uaminifu, uwazi, ubunifu, bidii ya kazi na moyo wa upendo na kujitolea. Ni kiongozi kijana anayetoa matumaini kwa vijana wenzake, wanawake, wazee na makundi maalum katika jamii.

Chichake anasema hatumii siasa kama jukwaa la sifa, bali kama nyenzo ya kuwahudumia watu, akisisitiza kuwa dira yake inalenga kujenga Tarime Vijijini yenye huduma bora za afya, maji, elimu bora na jumuishi, miundombinu inayowezesha biashara na uzalishaji, pamoja na fursa za kiuchumi kwa kila kijana na mwananchi wa kawaida.

Ameonesha kuwa ana mipango mahsusi ya kusaidia wajasiriamali wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini, kuinua kilimo na ufugaji kwa njia ya kisasa na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali ili kutengeneza ajira na kipato.

“Ninajua vipaumbele vya wananchi wetu na suluhisho la changamoto zinawakabili,” anasema Chichake.

Anaaminika kuwa kiongozi mwenye kipawa cha asili cha kuhamasisha, kushirikisha na kuunganisha jamii kwa msingi wa mshikamano na malengo ya pamoja. Ni mwepesi wa kusikiliza, mchambuzi wa hoja na mfuatiliaji wa utekelezaji wa ahadi. Haogopi changamoto, bali huzigeuza kuwa fursa.

Pambazuko jema
la Tarime Vijijini
Ni wazi kuwa kwa miaka mingi, wananchi wa Tarime Vijijini wamekuwa na kiu ya kuwa na mbunge anayewawakilisha si kwa maneno tu, bali kwa vitendo vinavyogusa maisha yao moja kwa moja.

Katika mwaka huu wa uchaguzi, jina la Nicolaus Mahando Mgaya “Chichake” limekuwa likitajwa kwa msisimko mkubwa katika mikutano ya kijamii, vijiweni na hata majukwaa ya kisiasa - kama chaguo jipya lenye matumaini ya pambazuko jema kwa wananchi wa jimbo Tarime Vijijini.

Ni kijana msomi anayekubalika kwa makundi yote ya jamii - vijana wenzake, wazee na akinamama, wakiwemo wajasiriamali, wakulima, wafugaji na watumishi wa umma.

Katika kipindi hiki ambacho taifa linahitaji viongozi wachapakazi, waadilifu na wabunifu - hasa kwa maeneo ya pembezoni kama jimbo la Tarime Vijijini, jina la Nicolaus Mahando Mgaya “Chichake” linaibuka kama nuru mpya inayoweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Kwa fikra pevu na moyo wa kujitolea, Chichake anawakilisha kizazi kipya cha viongozi wanaohitajika, wenye ujasiri, uthubutu wa kusikiliza, kusimamia rasilimali kwa uadilifu na kuchochea mabadiliko chanya. Mwenyewe anasema anastahili kuaminiwa na kupewa ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa jimbo la Tarime Vijijini kwa ufanisi mkubwa.

“Ni wakati sasa kwa wana-Tarime Vijijini kufanya chaguo jema la kunipa nafasi mimi kijana wao mwenye ndoto ya kweli ya kuleta pambazuko la mafanikio ya kisekta katika jimbo hili. Ninawaahidi niko tayari kuwatumikia kwa uadilifu na uaminifu mkubwa pasipo kuwaangusha,” anasema Chichake.

Kutoka jasho la vibarua
hadi kufanikiwa kiuchumi
Katika taswira ya maisha yenye mafunzo na msukumo kwa kizazi kipya cha Watanzania, simulizi ya Nicholaus Mahando Mgaya “Chichake” inasimama kama mfano halisi wa uthubutu, bidii na imani isiyoyumba katika ndoto ya kufikia maendeleo ya kiuchumi.

Harakati zake za kujikwamua zilianza katika mazingira magumu – akifanya kazi za vibarua vya ujenzi kwa jasho na maumivu, kisha akaingia kwenye biashara ya kusafirisha mikungu ya ndizi kwa kutumia baiskeli kutoka mashambani.

Baada ya hapo, Chichake anasema alianza kukaanga chips mitaani, umachinga wa kutembeza viatu mitaani, kulima mbogamboga, kabla ya kuendesha biashara ya kuku ambapo alikuwa akiwafuata kutoka Handeni - Tanga na Singida kupeleka kuwauza jijini Dar es Salaam.

Maelezo hayo siyo hadithi ya kawaida. Ni ushahidi kuwa mafanikio si zawadi ya bahati, bali ni matokeo ya kujituma, kuwa na maono na kutokata tamaa, hasa kwa kijana wa Kitanzania anayeamini kuwa maisha bora yanaanza na jasho lake mwenyewe.

Chichake anasisitiza kuwa katika safari yake ya kutafuta maendeleo ya kiuchumi hakuwahi kukata tamaa, ndiyo maana leo hii, anaweza kuajiri vijana wenzake, kuwapa matumaini na mwelekeo.

Hakika, Chichake anasimama si tu kama kielelezo cha mafanikio binafsi, bali pia kama mhimili mkubwa wa ajira kwa makundi ya wananchi, wengi wao wakiwa vijana wa kiume na kike ambao wameoajiriwa katika miradi yake ya kiuchumi.

“Nilianzisha kampuni zangu ambazo zimeajiri mamia ya vijana na kuleta maendeleo katika jamii,” anasema Chichake.

Alivyosaidia jamii
kiuchumi, kijamii
Chichake amejizolea umaarufu mkubwa katika jamii inayomzunguka kutokana na jitihada zake za kuwapunguzia kama si kuwaondolea wananchi changamoto zinazowakabili.

Moja ya makundi aliyosaidia ni watu waliopata madhara ya kujeruhiwa na kupoteza ndugu na wenza wao katika maeneo ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, ambapo aliomba Idara ya Mahusiano ya mgodi huo kufanya nao maridhiano.

“Pamoja na misaada mingine ya kibinadamu, nilishawishi mgodi ukakubali kuwapa wananchi hao mafunzo ya ufugaji, useremala na ushonaji ambayo yaliwasaidia kujiajiri na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao.

“Pia, nilishawishi mgodi ukatoa vifaa vya ujenzi na mtaji wa biashara ndogondogo kusaidia familia zilizoathirika, ambapo vijana 40 walinufaika na misaada hiyo kati ya mwaka 2013 na 2017,” anasema Chichake.

Mwaka 2008 hadi 2011, Chichake alikuwa Katibu Mkuu wa TAHESA iliyosimamia vijana waliokuwa wakisoma katika vyuo mbalimbali nchini kwa ufadhili wa mgodi wa North Mara.

“Vijana 150 walinufaika na fursa hiyo, na kwa sasa wengi wao wameajiriwa kwenye taasisi mbalimbali,” anasema Chichake.

Aidha, Chichake ameanzisha na kuendesha kampuni na miradi mbalimbali ya kiuchumi na kutengeneza ajira kwa mamia ya wananchi, wengi wao wakiwa vijana wa kiume na kike.

Baadhi ya miradi hiyo na idadi ya walioajiriwa ikiwa kwenye mabano ni Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Company Ltd (150) na mradi wa ufugaji wa nguruwe na uuzaji wa nyama ya mifugo hiyo kwenye mgodi wa North Mara (30).

Anamiliki pia Duka la Chichaka Hardware linalouza vifaa vya ujenzi na pikipiki, ambapo wameajiriwa vijana sita, mradi wa Chichake Sports Bar & Grill ulioajiri vijana wa kike na kiume wapatao 60 na Chichake Lodges ulioajiri watu 10.

Miradi mingine na idadi ya waajiriwa ikiwa kweye mabano ni Chichake Cartage Service (12), Pool Table (10) na Wakala wa M-Pessa (vijana wanne).

Zaidi ya hayo, Chichake ameanzisha mradi wa kuwakopesha vijana pikipiki kwa ajili ya biashara ya kusafirisha abiria (bodaboda) kwa makubaliano ya kulipa taratibu.

“Vilevile, tunawakopesha wafanyakazi wetu vifaa vya ujenzi bila riba na kuwapa elimu ya matumizi bora ya fedha na kujiwekea akiba.

“Sisi (Kampuni ya Chichake) ni wakandarasi wakubwa wanao- supply vijana wa kazi kwenye mgodi wa North Mara, lakini pia tunasaidia vijana kupata ajira mgodini.

“Pia, tunahamasisha vijana kuacha uvamizi mgodini na kuwasaidia njia za kufanya kazi halali ili kujipatia kipato, na wengi wao wameweza kuacha uhalifu huo na tayari wameanzisha biashara zao halali,” anasema Chichake.

“Lakini pia, tumesaidia vijana kuunda vikundi na kuibua miradi ya kiuchumi katika vijiji vinavyozunguka mgodi, na wakati mwingine tunavipatia ufadhili,” anaongeza.

Aidha, kwa sasa Chichake anasomesha mwanafunzi wa chuo anayetoka familia isiyojiweza, ambapo anamlipia gharama za masomo kiasi cha shilingi 70,000 kwa mwezi.

Lakini pia, Chichake anafadhili Mashindano ya Mpira wa Miguu ya Kemanyanki Cup yanayoshirikisha timu za vijana kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara.

Pia, ni mwaka wa pili sasa Chichake anajitolea kulipa shilingi 300,000 kila mwezi kwa ajili ya mwalimu wa masomo ya sayansi kwa lengo la kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Nyamongo.

Ikumbukwe pia kwamba Nicolaus Mahando Mgaya “Chichake” ni msomi wa chuo kikuu ambaye baada ya kuhitimu masomo yake hakutaka kuajiriwa, bali alirudi Nyamongo kushirikiana na jamii kutengeneza fursa za ajira kwa wengi.

Michango ndani
ya CCM na jamii
Chichake anatajwa kuwa miongoni mwa vijana wachache wenye rekodi adhimu ya kusaidia jamii hata kabla ya kupata Madaraka.

Kwanza, amekuwa mwanachama mtiifu wa CCM na anayeshiriki kufanikisha shughuli mbalimbali za chama hicho. “Mimi ni mwanachama mtiifu wa CCM, familia yangu ni CCM tangu nizaliwe hadi leo,” anasema.

Chichake alishiriki kikamilifu katika kampeni za kupata madiwani na wenyeviti katika kata ya Kemambo na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Pia, aliweza kusaidia kupata wanachama wapya 200 wa CCM katika kata ya Kemambo na kuwalipia gharama za kadi zao za uanachama.

Chichake pia amekuwa akichangia ujenzi wa ofisi za CCM katika kata mbalimbali Tarime Vijijini, lakini pia amekuwa akijitolea kuchangia fedha kufanikisha shughuli za chama hicho ngazi ya kata, wilaya na mkoa.

Chichake ameweza kujitolea kutoa msaada wa kompyuta yenye thamani ya shilingi 500,000 kwa Shule ya Msingi Matamankwe na kuchangia ujenzi wa Ofisi ya CCM Gwitiro saruji mifuko mitano.

Hali kadhalika, amechangia ujenzi wa Ofisi ya CCM Kijiji cha Itiryo saruji mifuko minne, Shule ya Msingi Kangariani saruji mifuko mitano na Ofisi ya CCM Ryagicheri (Ng'ereng'ere) saruji mifuko mitano.

Vilevile, amechangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Ng'ereng'ere saruji mifuko minne, Ofisi ya CCM Sirari (Remagwi, Nyabichune) saruji mifuko mitano na Kituo cha Afya Ganyange saruji mifuko saba.

Chichake pia amechangia ujenzi wa Stendi ya Borega A saruji mifuko mitano, Ofisi ya CCM Ntagacha saruji mifuko mitano, Shule ya Msingi Gorong'a saruji mifuko miwili na Ofisi ya Kijiji cha Masanga saruji mifuko mitano.

Aidha, amefadhili Mradi wa Kuku wa Umoja wa Vijana Sirari kwa msaada wa chakula cha kuku kilo 75 zenye thama ya shilingi 150,000 na ujenzi wa Shule ya Msingi Kwihancha saruji mifuko mitano.

Michango mingine ambayo Chichake ametoa ni saruji mifuko mitano kuchangia ujenzi wa Shule ya Msingi Gorong'a, Shule ya Sekondari Itiryo (saruji mifuko mitano) na Shule ya Msingi Itiryo (saruji mifuko miwili).

Ametoa michango kwenye makanisa mbalimbali kama vile S.D.A Susuni (shilingi 100,000), A.G.T Susuni (shilingi 100,000), Pemba (shilingi 100,000), RC Sirari (shilingi 100,000) na Kangariani (saruji 10).

Aidha, mwaka 2019, Chichake alishirikiana na Mgodi wa Dhhabu wa North Mara kufadhili Mbio za Mwenge wa Uhuru katika wilaya ya Tarime.

Hakika, Nicolaus Mahando Mgaya “Chichake” ni sauti ya kizazi kipya, kielelezo cha matumaini mapya na daraja la maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na vijavyo. Chichake ni kijana wa kazi. Chichake ni chaguo la mabadiliko. Chichake ni Tarime Vijijini mpya yenye ustawi wa jamii nzima. Chichake anatosha kupewa nafasi ya ubunge kwa mustakabali mwema wa wananchi wote.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages