
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akitoa maelekezo kwa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 mjini Mugumu, Serengeti juzi.
----------------------------------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ametoa msimamo wa serikali, akimtaka mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti, kuhakikisha anaukamilisha kwa muda uliopangwa bila visingizio.
Mradi huo unatekelezwa na mkandarasi Mega Engineering and Infrastructure Company Limited kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni 21 zilizotengwa na serikali.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo juzi, Kanali Mtambi alisema serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakandarasi, ikiwemo kutoa fedha kwa wakati na kuondoa vikwazo vya utekelezaji, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huo.

"Nimefurahishwa na maendeleo niliyoyaona hapa leo. Ni dhahiri mkandarasi anajitahidi na serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji safi na salama karibu na makazi yake.
“Mradi huu ulitakiwa kukamili Aprili, mkaomba kuongezewa muda mpaka Desemba [2025], hivyo mjue kabisa hakutakuwa na muda wa nyongeza, fedha ipo… nataka kuona unakamilika kwa wakati," alisema Kanali Mtambi.
Aidha, aliwahimiza wahandisi na wasimamizi wa mradi huo kuendelea kushirikiana kikamilifu na mkandarasi, huku wakihakikisha ubora wa kazi unazingatiwa kwa viwango vya kitaalamu ili uakisi thamani halisi ya fedha (value for money) kwa manufaa endelevu ya wananchi.
Kwa upande mwingine, aliwataka wananchi wa Serengeti kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalamu na wafanyakazi wa mradi huo, lakini pia kutunza miundombinu ya mradi huo utakapokamilika ili uweze kuleta tija iliyokusudiwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa inaakisi uwajibikaji unaolenga kukomesha kasumba ya wakandarasi wanaotumia muda wa ziada bila tija, hali inayokwamisha maendeleo ya wananchi waliotarajia manufaa ya haraka kutoka kwa miradi ya kijamii.

Kwa kuzingatia kuwa mradi huo utakapokamilika utahudumia maelfu ya wakazi wa mji wa Mugumu na vijiji jirani, serikali imedhamiria kuhakikisha hakuna mianya ya uzembe, ubadhirifu au uzorotaji unaoweza kuvuruga dhamira hiyo ya maendeleo.
Wakazi wa mji wa Mugumu wameonesha matumaini makubwa kwa mradi huo, wakiamini kuwa kukamilika kwake kutaleta mapinduzi makubwa katika maisha yao - kwa kuwapunguzia adha ya muda mrefu ya uhaba wa maji safi na salama.
Hata hivyo, wameitaka serikali kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi kama hiyo na kusisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi nao ni sehemu ya mafanikio ya miradi ya kijamii.
Mradi wa Maji wa Miji 28 katika mji wa Mugumu - Serengeti unaogharimu shilingi zaidi ya bilioni 21, ulianza kutekelezwa Aprili 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2025, ambapo unatarajiwa kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wakazi zaidi ya 100,000 wa mji wa Mugumu na vijiji jirani.
Hivyo, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kuboresha zaidi huduma ya maji katika maeneo hayo.
Mbali na kupunguza tatizo la uhaba wa maji, mradi huo unatarajiwa kuongeza shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kuwawezesha wananchi kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji badala ya kutafuta maji.
Hatua ya Mkuu wa Mkoa huyo kutoa msimamo wa serikali kwa mkandarasi wa mradi huo wa maji ni mfano wa uongozi wa uwajibikaji na uwazi unaohitajika kwa kasi ya maendeleo na uboreshaji wa maisha ya wananchi kwa vitendo.
Vilevile, wito wake wa kuwahimiza wananchi kushiriki kulinda miundombinu ya maji unaendana na falsafa ya maendeleo shirikishi, ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikiisisitiza.
No comments:
Post a Comment