Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, leo imekutana jijini Dodoma kwa uteuzi wa wagombea Ubunge wa Majimbo na Viti Maalum wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe wake wa Viti Maalum kwa upande wa Zanzibar.
Kikao hicho cha Kamati Kuu kitafuatiwa Jumamosi na kikao cha Halmashauri Kuu ambacho kitapitisha orodha ya majina ya wagombea waliopendekezwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025 utakaafanyika Oktoba 29.
Huu utakuwa ni Uchaguzi Mkuu wa saba tangu Tanzania iingie kwenye mfumo wa vyama vingi hapo Julai 1, 1992, kutokana na wimbi la mageuzi ya kisiasa yalilolikumba bara la Afrika katika miaka ya 1990.
Majina ya wagombe Ubunge wa Majimbo na Viti Maalum kwa upande wa Tanzania Bara na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wale wa Viti Maalum kwa upande wa Zanzibar yanatarajiwa kutangazwa rasmi Jumamosi Agosti 23, 2025 baada ya kumalizika kwa kikao cha Halamshauri Kuu ya CCM.
Mpaka sasa, haijulikani ni lini vyama vya upinzani vitataja majina ya wagombea wao kwenye mchuano huo wa kuingia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano au Baraza la Wawakilishi.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kampeni za miezi miwili za wagombea wa nafasi za Urais, Ubunge, na Udiwani zinatarajiwa kuanza rasmi Alhamis Agosti 28, 2025 na kumalizika Oktoba 28, ambayo itakuwa siku ya mkesha wa Uchaguzi Mkuu.
No comments:
Post a Comment