Dkt Asha Rose Migiro
Na Mwandishi Wetu
Kwa mara ya kwanza katika historia, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeandika historia baada ya kumteua Dkt Asha-Rose Migiro kuwa Katibu Mkuu wake wa kwanza mwanamke tangu kianzishwe mwaka 1977 baada ya kuviunganisha vyama vya ukombozi vya TANU kwa upande wa Tanzania Bara na Afro-Shiraz kwa upande wa Zanzibar.
Katika uhai wake wa miaka 48, CCM imekuwa ikiongozwa na Makatibu Wakuu wanaume kuanzia Mzee Pius Msekwa hadi Dkt Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni mgombea mwenza wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba 29.
Dkt Migiro ni mwanamama mwanazuoni aliyebahatika kupata uzoefu wa kufanya kazi za kimataifa alipoteuliwa na Katibu Mkuu wa nane wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chombo hicho cha kimataifa.
Ban Ki-Moon aliongoza Umoja wa Mataifa kwa miaka minane kuanzia 2007 hadi 2016 alipomaliza muda wake.
Kabla ya kuingia kwenye uongozi wa serikali pale alipoteuliwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Dkt Migiro alikuwa Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alizidi kupata uzoefu zaidi katika diplomasia ya kimataifa baada ya Rais hayati John Pombe Joseph Magufuli kumteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, ambayo ni mtawala wa kikoloni wa iliyokuwa Tanganyika baada ya kumalizika kwa Vita ya Kwanza ya Dunia hadi kupatikana kwa uhuru Desemba 9, 1961.
Uteuzi wa Dkt Migiro kuwa Katibu Mkuu wa CCM unaamanisha nini?
Hili ndilo swali la msingi wanalouliza watu wengi lipokuja suala la uhusiiano wa kijinsi baina ya wanaume na wanawake. Ni sswali ambalo Watanzania wengi hulikwepa kulijibu kwa ufasaha na kwa kina.
Lakini wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema kumteua CCM Dkt Migiro kuwa Katibu Mkuu wa CCM ni kuwapa wanawake sauti katika harakati za maendeleo ya taifa, hasa baada ya miongo mingi ya mfumo dume ambao ulionekana kuwapendelea wanaume inapokuja kwenye suala la jinsia.
Wanasema huenda Dkt Migoro akawa kipaza sauti cha wanawake katika utoaji maamuzi muhimu ya maendeleo ya taifa bila bila ubaguzi.
Pengine uteuzi wake pia umezingatia ukweli kwamba kitakwimu wanawake ndio asilimia kubwa ya Watanzania wote wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 60 kwa mujibu wa Sense ya Watu na Makazi ya 2022.
Hali kadhalika, hakuna ubishi kwamba wanawake ndiyo wapiga kura wengi nchini Tanzania lipokuja suala la uchaguzi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa.
Inatarajiwa kwamba kwa mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu, Dkt Migiro atakuwa kichocheo kikubwa cha kuwahamasisha wanawake wapige kura katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika harakati za kudai uhuru miaka ya 1950 na baada ya uhuru kulikuwepo wanawake waliojitoa mhanga kupinga ukoloni kwa kuwa bega kwa bega na uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Wachambuzi wa masuala ya kijinsia wanasema kuteuliwa kwa Dkt Migiro kuongoza chama tawala kutaunganisha juhudi na mchango wa wanawake katika maendeleo kwa kila sekta ili Tanzania izidi kuimarisha uchumi wake.
Kwa wadadisi wa harakati za maendeleo tangu kupatikana kwa uhuru zaidi miaka 60 iliyopita, wanawake ndiyo wazalishaji wakubwa katika sekta ya kilimo ingawa maisha yao yameendelea kuwa duni.
Katika Tanzania, kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika, wanawake ndiyo nguzo ya familia nyingi ingawa mchango wao hauthaminiwi kwa kiasi kikubwa, jambo linalowafanya waendelee kuelea katika dimbwi la umaskini.
Kwa hiyo, uteuzi wa wanawake katika nafasi za ngazi juu za utawala, iwe serikali au kwenye vyama vya siasa, ni lazima ulete mageuzi ya kuwakomboa wanawake na janga la umaskini ili kuwapunguzia mzigo unaowaelemea wa kuhudumia familia zao.
Wakati huo huo uteuzi wa Dkt Migiro umekuja na umefuatana na kuteuliewa kwa Katibu mpya wa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, ambaye anachukua nafasi ya aliyekuwa mtangulizi wake Amos Makalla ambaye sasa atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Katika uteuzi huo, CCM pia imempata Katibu wa NEC Uchumi na Fedha mpya,Joshua Chacha Mirumbe.
No comments:
Post a Comment