
Luhaga Joelson Mpina
Chama cha ACT Wazalendo kimemuidhinisha rasmi Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Uamuzi huo umefikiwa na Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam, ambayo ilipendekeza majina mawili, Aaron Kalikawe na Luhaga Mpina.
Majina hayo yaliyopendekezwa yaliwasilishwa kwa Mkutano Mkuu Taifa kwa ajili ya kupigiwa kura, ambapo katika mkutano huo, Mpina alichaguliwa kwa kishindo kwa kupata kura 559 sawa na asilimia 92.3 ya kura zote 610 zilizopigwa.
Mpina amemshinda mgombea mwenzake Kalikawe aliyepata kura 46 sawa na asilimia 7.7, na sasa atapeperusha bendera ya ACT katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, mgombea mwenza akiwa Fatma Ferej.
Kwa upande wa Zanzibar, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amechaguliwa kuwa Mgombea Urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupata kura 606 za ndiyo sawa na asilimia 99.5 ya kura zote halali 609.
Mpina ni nani?

Mpina akiwa bungeni
Luhaga Joelson Mpina alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kisesa mkoani Simiyu. Mwaka 2005 alichaguliwa mara ya kwanza kuwa mbunge akarudishwa katika chaguzi za 2010, 2015 na 2020.
Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano mwaka 2015-2017, baadaye mwaka 2017-2020 alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Mpina amekuwa pia mjumbe kwenye kamati mbalimbali za bunge, ikiwemo ya fedha na uchumi, viwanda na biashara na kamati ya bajeti.
Mpina ambaye ni mtaalam wa fedha ana shahada mbili kwenye sekta hiyo; moja akipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyingine Chuo Kikuu cha Strathclyde nchini Uingereza.
Ameshawahi kufanya kazi kama Afisa Mtendaji wa Kata huko Meatu, Simiyu mwaka 1999-2000 na Mhasibu wa Daraja la Pili.
Kwenye chama chake cha zamani, CCM, Mpina amewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Meatu kwa miaka mitano - mwaka 2003-2008.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment