NEWS

Thursday, 7 August 2025

Tanzania yajiweka pazuri kuelekea robo fainali michuano ya CHAN 2024



Wachezaji wa Taifa Stars, Kapombe (kulia) na Mzize wakishangilia ushindi jana.
------------------------------------

Wenyeji Tanzania wamejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania, bao lililofungwa dakika za lala salama na beki mkongwe Shomari Kapombe.

Mchezo huo wa Kundi B ulifanyika jana Jumatano usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo mashabiki walishuhudia dakika 88 za mvutano kabla ya Kapombe kufunga bao hilo - akimalizia pasi ya kiufundi kutoka kwa Iddy Nado na kumtungua kipa Abderrahmane Sarr, na kuzua shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki wa nyumbani.

Ushindi huo unakuwa wa pili kwa Taifa Stars katika mechi mbili za mwanzo, na sasa wanaongoza Kundi B kwa alama sita bila kuruhusu bao lolote - hatua inayowaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano.

Kwa upande wa Mauritania, hali si shwari kwani bado hawajapata ushindi wowote na sasa wanakabiliwa na kibarua kigumu kusalia kwenye michuano hiyo.

Mudathir Yahya nyota wa mchezo

Mudathir Yahya akipokea 
tuzo ya nyota wa mchezo.
------------------------------------

Katika ushindi huo wa pili mfululizo kwa Tanzania, Mudathiri Yahya, kiungo fundi wa Taifa Stars, aliibuka kuwa mhimili wa timu na mchango wake ukamfanya atangazwe kuwa Mchezaji Bora wa Mechi (Total Energies Man of the Match).

Mudathir ambaye mara nyingi hufananishwa na "moyo wa timu", alikuwa muhimili katika mfumo wa kocha Hemed Suleiman, akiongoza mashambulizi na kuimarisha safu ya ulinzi kwa nidhamu ya hali ya juu.

Akizungumza baada ya mechi, Mudathir alisema: "Tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunafuzu hatua ya mtoano tutachukua kila mechi kwa uzito wake." Kauli yake inaonesha dhamira ya kikosi cha Taifa Stars kutimiza malengo yake hatua kwa hatua.

Akiwa na umri wa miaka 29, Mudathir ni mmoja wa wachezaji wakongwe kwenye kikosi cha Tanzania.

Alisisitiza umuhimu wa wachezaji wenye uzoefu katika mashindano ya kiwango cha juu kama CHAN akisema: "Uzoefu ni jambo la msingi. Katika mechi ngumu, timu kubwa huhitaji wachezaji waliokomaa. Hawa huwapa moyo vijana na kwa pamoja tunalenga ushindi."

Kwa maneno haya, Mudathir anaonesha kuwa kiongozi si kwa kucheza pekee, bali pia kwa kuwalea na kuwaongoza wachezaji chipukizi.

Kwa kiwango chake hadi sasa, Mudathir anaonekana kuwa kiongozi mwenye maono, uzoefu na morali ya ushindi mambo yanayoipa Tanzania matumaini makubwa katika CHAN 2024.

Tanzania sasa inaongoza Kundi B ikiwa na alama sita baada ya mechi mbili, bila kuruhusu bao.

Burkina Faso inafuata kwa alama 3, huku Madagascar na Mauritania kila mmoja akiwa na alama mmoja. Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) bado haijakusanya pointi lakini ina mechi moja mkononi.

Kwa Tanzania, hali hii inawaruhusu kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wao muhimu katika mchezo ujao dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kabla ya kukamilisha ratiba ya kundi kwa kumenyana na Madagascar.

Kwa Mauritania, hali ni ngumu wanahitaji ushindi wa lazima dhidi ya Burkina Faso na kusubiri matokeo mengine yaende kwa faida yao.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages