NEWS

Thursday, 14 August 2025

Mtambi ajivunia ujio wa TACTIC, asema itaboresha mandhari ya Musoma



Mkuu wa Mkoa wa Mara,
Kanali Evans Alfred Mtambi.
----------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amejivunia ujio wa TACTIC akisema utabadilisha mandhari ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kuwa na muonekono mzuri zaidi.

Kanali Mtambi aliyasema hayo mjini hapa juzi wakati wa hafla ya utiaji saini ujenzi wa Miradi ya Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC) katika Manispaa ya Musoma itakayogharimu shilingi bilioni 19.975.

Miradi ya TACTIC inatekelezwa katika miji 45 Tanzania kwa udhamini wa Benki ya Dunia (WB).

“Binafsi nina furaha kubwa, maana ujenzi wa miradi hii ikiwamo Soko la Nyasho, barabara za ndani ya Manispaa na Stendi ya Bweri itasaidia kubadilisha muonekano wa Manispaa ya Musoma,” alisema Kanali Mtambi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Aliongeza kuwa miradi hiyo itakapokamilika italeta mabadiliko chanya kwa wananchi na wageni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara, kupandisha thamani ya maeneo husika na kuongeza mapato ya Manispaa ya Musoma.

Hivyo, aliwataka viongozi na wataalamu kuisimamia vizuri miradi hiyo, ambapo alimtaka mkandarasi MS Henan Highway Engineering Group Company Limited kuikamilisha mradi aliopewa kwa wakati na kwa ubora kulingana na mkataba husika.

Awali, akitoa taarifa ya miradi hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Bosco Nduguru, alisema inatarajiwa kutekelezwa kwa muda wa miezi 15 kuanzia Agosti 15 hadi Novemba 2026, ambapo itahusisha ujenzi wa miradi mikubwa mitatu na ofisi za usimamizi na uratibu wa ujenzi wa miradi hiyo.

Nduguru alisema miradi itakayojengwa katika Manispaa ya Musoma kupitia mradi wa TACTIC ni pamoja na barabara tatu za Mukendo, Shaabani na Musoma Bus –Saanane, Soko la Nyasho na Stendi ya Bweri.

Wakati huo huo, Kanali Mtambi amewahamasisha wananchi wa Manispaa ya Musoma kushiriki mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika mkoani Mara kuanzia Agosti 15 hadi 23, 2025.

Aidha, amewahamasisha wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu kuanzia kwenye kampeni hadi kupiga kura Oktoba 29, 2025 ili kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages