NEWS

Friday, 15 August 2025

Mwenge wa Uhuru 2025 wawasili Mara, kukimbizwa kwenye halmashauri 9




Na Mwandishi Wetu, Bunda

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya, leo Agosti 15, 2025 amepokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Prisca Joseph Kayombo, kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Balili katika Halmashauri ya Mji wa Bunda.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Kusaya amesema Mwenge ukiwa Mara utakimbizwa umbali wa kilomita 1,123 katika halmashauri zote tisa za mkoa huo hadi Agosti 23, 2025 kisha kuelekea mkoani Mwanza siku itakayofuata.

Ameongeza kuwa Mwenge huo utatembelea miradi 68 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 26,547,598,285 katika sekta za elimu, afya, maji, ujenzi, kilimo, mifugo, mazingira, ustawi wa jamii, viwanda na biashara katika halmashauri hizo.

Pia, Mwenge huo utapita nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwitongo wilayani Butiama ambapo Agosti 18, 2025 utapata nafasi ya kuwasha Mwenge wa Mwitongo.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ukiwa Mwitongo utapata nafasi ya kuzuru na kuweka mashada ya maua katika Kaburi la Baba wa Taifa na kutembelea Makumbusho ya Baba wa Taifa na kupata historia ya Baba wa Taifa,” amesema Kusaya.

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 ni “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”

Kusaya ametumia nafasi hiyo pia kuwahamasisha wananchi wa mkoani Mara kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kuwachagua viongozi watakaoliongoza taifa kwa miaka mitano ijayo.

Amesema mkoa wa Mara umejipanga vizuri kuelekea uchaguzi huo, ambapo tayari wasimamizi wa uchaguzi huo ngazi ya jimbo wamepatiwa mafunzo ya usimamizi wa uchaguzi na mafunzo ya wasimamizi ngazi ya kata yanaendelea.

Aidha, Kusaya amewataka wananchi kutunza kadi ya mpiga kura, kushiriki katika mikutano ya kampeni ili kuwasikiliza wagombea, kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, kuheshimu, kuzingatia katiba, sheria, kanuni na maelekezo yatakayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kuepuka vitendo vya rushwa na kushirikiana na viongozi watakaochaguliwa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages