NEWS

Saturday, 23 August 2025

RC Mtambi, viongozi wa dini Mara wakutana, wahamasisha udumishaji amani kuelekea Uchaguzi Mkuu



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini wajumbe wa Kamati ya Amani na Maridhiano ya mkoa huo - mjini Musoma jana.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika nchini Oktoba 29, 2025.

Akizungumza katika kikao cha viongozi wa kiroho ambao pia ni wajumbe wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara - kilichofanyika mjini Musoma jana, Kanali Mtambi alisema wana jukumu kubwa la kuwaongoza waumini wao kumtanguliza Mungu katika mambo yote kipindi hiki muhimu ili Watanzania waweze kuvuka salama wakiwa katika umoja, amani na mshikamano.

“Muwahimize waumuni watambue kuwa bila ya kumtanguliza Mwenyezi Mungu utandawazi na wanasiasa wasio na nia nzuri na taifa letu wanaweza kutuvuruga kwa kutumia mitandao ya kijamii, lakini tukimtanguliza Mungu tutakuwa na umoja na mshikamano wetu,” alisema.

Kanali Mtambi alitumia nafasi hiyo pia kuwashukuru viongozi hao kwa namna walivyotoa ushirikiano katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 ambapo ilishuhudiwa kupanuka kwa demokrasia na ukomavu wa kisiasa uliowezesha uchaguzi huo kufanyika kwa amani na utulivu.

Pia, aliwashukuru viongozi hao kwa kuandaa kikao hicho kujadiliana mambo muhimu kwa mwaka huu ili uchaguzi ufanyike katika hali ya amani na utulivu, na akawaomba kuendelea kuitisha vikao vya aina hiyo kwa ajili ya kupeana hamasa ya kulinda amani.

“Ninawaomba tushirikiane ili tufanye vizuri katika uchaguzi huu kuliko mwaka jana, ili wananchi wetu waendelee kupambana kujenga uchumi wao kwani hawawezi kujenga uchumi kama hamna amani na utulivu,” alisisitiza Mtambi.

Kiongozi huyo wa mkoa alisisitiza pia umuhimu wa waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini kuhamasishwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi na kwa wale wenye sifa kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara, Sheikh Juma Masiroli, alisema viongozi wa dini katika mkoa huo kwa umoja wao watakwenda kwenye nyumba za ibada kuzungumza na waumini wao na kuliombea taifa ili nchi ivuke salama.

Mwenyekiti wa Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara, Askofu Jacob Rutubinga, naye aliwahimiza viongozi wa dini kuhakikisha kuwa mkoa huo unaongoza kwa amani na utulivu wakati wote wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ili mikoa mingine ije kujifunza namna ya kulinda amani na utulivu wakati wa uchaguzi.

Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi, kwa ushirikiano anaowapa viongozi wa dini wa katika mkoa huo unaopakana na nchiu ya Kenya.

Sheikh wa Mkoa wa Mara, Msabaha Kassimu, yeye alitumia nafasi hiyo kutoa wito wa kuwakumbusha Watanzania kutambua kuwa kila mtu ana wajibu wa kuilinda amani na utulivu vilivyopo nchini wakati wote.

Naye Naibu Askofu Jimbo Katoliki Musoma, Padri Julius Auko Ogolla, alisema kwa kutambua umuhimu wa nchi kuwa na amani na utulivu, Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC) limeelekeza kanisa kufanya mafungo ya saa 24 kuanzia Agosti 22 hadi 25, mwaka huu kwa ajili ya sala za kuombea amani Uchaguzi Mkuu ujao.

Kikao hicho cha Kamati ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Mara kilihitimishwa kwa viongozi wa dini walioshiriki kikao hicho kukubaliana kuandaa ibada ya pamoja kwa ajili ya kuliombea taifa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu uweze kufanyika kwa amani na utulivu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages