Bethel Park, kitongoji kidogo cha Pittsburgh katika jimbo la Pennsylvania kinatetemeka baada ya FBI kumtaja kijana wa eneo hilo, Thomas Matthew Crooks, kuwa ndiye aliyemshambulia kwa risasi Donald Trump wakati wa mkutano wa kampeni na kulishtua taifa zima.
Crooks, akiwa na bunduki aina ya AR-15 kutoka kwenye paa la jengo, alimfyatulia risasi rais huyo wa zamani wa Marekani alipokuwa akihutubia umati wa watu huko Butler, Pennsylvania, na kusababisha mhudhuriaji mmoja kuuawa na wengine wawili kujeruhiwa.
Mfanyakazi huyo wa jikoni mwenye umri wa miaka 20 alipigwa risasi na kufa katika eneo la tukio na mdunguaji wa Secret Service.
Katika mji wake, majirani wako katika mshtuko, wakishindwa kuelewa jinsi kijana mkimya alivyoingia kwenye kesi ya kumpiga risasi Trump.
Thomas Matthew Crooks hakuwa amebeba kitambulisho, kwa hivyo wachunguzi walitumia DNA na teknolojia ya utambuzi wa uso kumtambua, FBI ilisema.
Ametokea Bethel Park, Pennsylvania, takriban kilomita 70 (maili 43) kutoka eneo la shambulio. Alihitimu 2022 katika Shule ya Sekondari ya Bethel Park na akapata zawadi ya Dola za Kimarekani 500 kwa kufanya vyema katika hisabati na sayansi.
Crooks alikuwa akifanya kazi kama mpishi katika nyumba ya uuguzi karibu na nyumbani kwake. Wafanya kazi wenzake wanasema, ukaguzi wa maisha yake haukuonesha kuwa alikuwa na tatizo lolote.
Chuo cha Community College of Allegheny, au CCAC, kimethibitisha kuwa Crooks alihudhuria masomo kati ya Septemba 2021 na Mei 2024. Alihitimu na shahada ya sayansi ya uhandisi.
Katika taarifa iliyotumwa kwa BBC, chuo hicho kilibainisha kuwa alifuzu "kwa daraja kubwa" na rekodi zake hazikuonesha utovu wa nidhamu, matukio mabaya au matukio yanayohusiana na usalama.
Rekodi serikali ya jimbo zinaonesha alisajiliwa kama mfuasi wa chama cha Republican, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.
Pia alitoa Dola za Kimarekani 15 kwa kikundi cha kampeni cha kiliberali kiitwacho ActBlue mwaka 2021, kulingana na jalada la mchango na ripoti za habari.
Alikuwa mwanachama katika klabu ya kulenga shabaha, iitwayo Clairton Sportsmen Club, kwa takriban mwaka mmoja, klabu hiyo ilithibitisha kwa BBC.
Klabu hiyo iko kusini mwa Pittsburgh na ina wanachama zaidi ya 2,000 katika majimbo matatu ya Pennsylvania, Ohio na West Virginia.
Maafisa wa upelelezi wanaamini silaha iliyotumiwa kumpiga Donald Trump, bunduki aina ya AR, ilinunuliwa na babake Crooks.
Haijulikani ni jinsi gani silaha hiyo iliingia mikononi mwa mwanawe, ingawa hakuna uthibitisho kwamba baba yake alikuwa na ufahamu wa shambulio hilo.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, maafisa wawili waliambia AP, babake Crooks alinunua silaha hiyo miezi sita iliyopita.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, Crooks alikuwa amevalia fulana la Demolition Ranch, chaneli ya YouTube inayojulikana kwa maudhui ya bunduki. Chaneli hiyo ina mamilioni ya wafuatiliaji.
Siku moja baada ya kupigwa risasi, maafisa wanasema vifaa vya kutiliwa shaka vilipatikana kwenye gari la Crooks. Maafisa wa kutegua mabomu waliitwa kwenye eneo la tukio ili kuchunguza vifaa hivyo.
Sababu za kufanya shambulio ni zipi?
Maafisa wakimwondoa Trump
baada ya kushambuliwa
Baada ya kutambua utambulisho wa Crooks, polisi na mashirika yanachunguza nia yake. Hadi sasa, hawajaweza kutambua sababu.
Julai 15, 2024, FBI ilisema wataalamu wake wa uchunguzi wamefanikiwa kupata simu ya Crooks, na wanaichunguza na kutafuta ushahidi mwingine.
“Uchunguzi wa kile kilichofanyika unaweza kudumu kwa miezi kadhaa na wachunguzi watafanya kazi bila kuchoka kubaini sababu ya Crooks ilikuwa ni nini,” anasema Kevin Rojek, afisa wa FBI huko Pittsburgh.
Familia ya Crooks inashirikiana na wachunguzi, kulingana na FBI.
Kwa mujibu wa vyanzo vitatu vya polisi, CBS imeripoti kuwa babake alipiga simu polisi baada ya shambulio hilo, ingawa haijulikani aina ya mazungumzo yaliyofanyika. Kwa jumla, zaidi ya mahojiano 100 hadi sasa yamefanywa.
Polisi walifunga barabara hadi kwenye nyumba ambayo Crooks aliishi na wazazi wake. Upekuzi wa makazi hayo ulikamilika Julai 15, 2024.
Jirani aliiambia CBS kuwa maafisa walimhamisha katikati ya usiku bila onyo.
Polisi wa Bethel Park walisema kulikuwa na uchunguzi wa bomu katika nyumba ya Crooks.
Njia ya kuingia eneo hilo bado inadhibitiwa na polisi, na gari la polisi limeziba barabara mbele ya nyumba hiyo. Wakazi pekee ndio wanaruhusiwa kuingia au kutoka mtaa huo.
Polisi wanaamini Crooks alitekeleza tukio hilo peke yake, lakini wanaendelea kuchunguza ikiwa aliandamana na mtu mwingine kwenda kwenye mkutano huo.
Alikuwa mtu wa aina gani?
Wakizungumza na chombo cha habari cha eneo hilo KDKA, baadhi ya wenyeji wa eneo hilo waliokwenda shuleni pamoja naye, walimtaja kuwa mtu mpweke, ambaye alibugudhiwa mara kwa mara na wakati mwingine alivaa nguo za kuwindia shuleni.
Mwanafunzi mwingine wa zamani wa darasa lake, Summer Barkley, ameiambia BBC, "kila mara alikuwa akipata alama nzuri kwenye masomo na alipenda sana historia.”
"Chochote kuhusu serikali na historia alionekana kujua," anasema Barkley. Anasema pia alipendwa sana na walimu wake.
Wengine wanamkumbuka kama mtu mkinya.
"Alikwa darasani siwezi kufikiria mtu yeyote ambaye alimfahamu vyema," anasema mwanafunzi mwenzake wa zamani, ambaye aliomba asitajwe jina.
Mwanafunzi mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina lake pia, anasema "alikuwa na akili lakini wa ajabu kidogo."
Alikuwa mtoto mzuri ambaye hakuwahi kumzungumzia vibaya mtu yeyote na sikuwahi kufikiria kuwa anaweza kufanya alichofanya siku chache zilizopita.
Max Smith, ambaye alichukua kozi ya historia ya Marekani na Crooks, aliiambia Philadelphia Inquirer, "alikuwa mhafidhina."
Smith anakumbuka mjadala ambapo wote wawili walishiriki, akisema: "Watu wengi walikuwa upande wa uliberali, lakini Tom, bila kujali nini, alisimama upande wake wa kihafidhina."
"Inanifanya nishangae kwa nini alitaka kumuua mgombea wa kihafidhina," anasema Smith.
Waathiriwa wengine ni nani?
Mtu mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa kwa risasi. Waathiriwa wote watatu ni wanaume watu wazima na walikuwa watazamaji.
Katika mkutano na wanahabari siku ya Jumapili, Gavana wa Pennsylvania, Josh Shapiro alimtaja mwathiriwa aliyefariki kuwa Corey Compperatore, mzima moto wa zamani wa kujitolea mwenye umri wa miaka 50 ambaye aliuawa wakati "akiikinga familia yake.” Alisema kuwa Compperatore "alikufa shujaa."
Watu wawili waliojeruhiwa katika shambulio hilo wametambuliwa kuwa ni David Dutch mwenye umri wa miaka 57 na James Copenhaver mwenye umri wa miaka 74. Wanaume wote wawili ni wakaazi wa Pennsylvania na wako katika hali nzuri.
Ukurasa wa GoFundMe, ulioandaliwa na mkurugenzi wa fedha wa kitaifa wa kampeni ya Trump, Meredith O'Rourke, umekusanya michango kwa familia za waliojeruhiwa, Dola za Kimarekani zaidi ya 340,000. BBC
UNAWEZA PIA KUSOMA:
- 1.HAIPPA PLC inavyoshagihisha uwekezaji Tanzania .
- 2. Musoma Vijijini wanavyopiga hatua ujenzi shule za sekondari za kata .
- 3.Rais Samia atembelea Sekondari ya Seminari ya Kaengesa mkoani Rukwa .
- 4.Waridi wa BBC: Rushwa ya ngono inazima ndoto za wasichana wengi .
- 5.Siasa:Nape aomba radhi kutokana na kauli yake ya ‘ushindi nje ya boksi’ .
No comments:
Post a Comment