NEWS

Sunday, 4 August 2024

WAMACU washusha bei ya mbolea kwa wakulima wa tumbaku Serengeti



Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye.
--------------------------------------------------


NA WAANDISHI WETU, Serengeti
------------------------------------------------

Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) kimesema bei ya mbolea ya tumbaku iliyosambazwa kwa wakulima wa wilayani Serengeti kwa msimu wa 2023/2024 baada ya WAMACU kuanza kuwahudumia wakulima katika wilaya hiyo.

“Mfano katika msimu wa mwaka 2023/2024 baada ya WAMACU kuingia, bei ya mbolea aina NPK yenye ujazo wa kilo 50 ilishuka kutoka Dola za Kimarekani 70.128 hadi dola 58.51,” Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU, Samwel Gisiboye alisema katika mahojiano na Mara Online News ofisini kwake jana.

Pia GM Gisiboye alitoa mfano wa mbolea ya CAN ambayo alisema baada ya wao kuanza huduma ya kusimamia usambazaji wa pembejeo kwa wakulima hao, ilishuka kutoka Dola za Kimarekani 65 hadi 45 kwa mfuko wa kilo 50.

“Haya kwetu kama WAMACU yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa wakulima wa tumbaku katika wilaya ya Serengeti kwa msimu wa 2023/2024,” alisema.

Aliongeza kuwa wakulima wa tumbaku wa wilayani Serengeti walipata mbolea kwa bei ya chini ukilinganisha na maeneo mengine nchini.

GM Gisiboye alitoa wito kwa wakulima wa tumbaku kuwapuuza watu aliowaita wapotoshaji wanaozusha uongo baada ya kubaini kuwa mianya yao ya ‘kuwapiga’ wakulima imezibwa kutokana na ujio wa WAMACU wilayani Serengeti.

Alidai kuwa baadhi ya viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) wanatengeneza ‘propaganda’ ili wakulima wasiendelee kufurahia matunda ya ushirika kupitia kwa WAMACU.

“Baadhi ya viongozi wanafanya haya [wa AMCOS] kwa maslahi yao binafsi baada ya kuona uwepo wa WAMACU wilayani Serengeti umeziba mianya ya kunyonya wakulima,” alisema GM Gisiboye.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa AMCOS hazilazimishwi kujiunga na WAMACU kama inavyodaiwa na baadhi ya viongozi wa AMCOS za wilaya hiyo.

Alisema AMCOS 18 kati 22 zinazojihusisha na kilimo cha tumbaku katika wilaya ya Serengeti ziliomba kujiunga na WAMACU na kupokewa na Mkutano Mkuu wa WAMACU.

“Hizi AMCOS zilipokewa tarehe 27 Januari, 2023 kwenye Mkutano Mkuu wa WAMACU ambao ulifanyika katika Hoteli ya Blue Sky mjini Tarime, na mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti wa wakati huo, Dkt Vincent Mashinji,” alifafanua GM Gisiboye.

Alisema AMCOS nne ikiwemo ya Miti Mia zilikuwa hazijapata usajili halali kwa wakati huo.

“Hata hivyo, AMCOS hizo nne ziko chini ya WAMACU ili kuwezesha wakulima kuendelea kupata huduma kutokana na ulazima wa zao la tumbaku, na tumekuwa tukifanya hivyo kwa maslahi ya wakulima,” alieleza.

Kwanini kampuni zilijitoa
kusambaza pembejeo

GM Gisiboye alisema kampuni mbili zilizokuwa zimeshinda kusambaza pembejeo ziliandika barua kujitoa baada ya kubaini kuwa mahitaji halisi yalikuwa chini ya idadi iliyokuwa imewekwa na AMCOS.

“Mahitaji yote yalibadilika kwa kushuka. Mfano, tulipotangaza tenda mahitaji ya mbolea ya NPK yalikuwa mifuko 10,376 lakini mahitaji halisi wakati wa kufunga mkataba yalishuka hadi mifuko 4,620, na mbolea ya CAN mahitaji yalishuka kutoka mifuko 2,594 hadi 1,800. Mahitai yote yalibadilika kwa kushuka hadi dawa zote,” alisema Gisiboye.

Kuna madai ambayo hayajathibitishwa kuwa baadhi ya AMCOS ziliweka makisio ya juu kwa lengo la kutaka kupiga ‘fedha’.

“Makisio ya juu kuliko uhalisia yalikuwa na ajenda ya siri, na walioweka hivyo wanajua walitaka kupata nini,” kilisema chanzo chetu cha uhakika kutoka wilayani Serengeti jana.

Kwa mujibu wa GM Gisiboye , baada ya kampuni mbili kujitoa, Kampuni ya Gimmy International ilifanya kazi hiyo kwa lengo la kuwafikishia wakulima huduma ya mbolea.

“Kwa sababu hatukuwa na muda wa kutangaza tenda tena, tuliamua kumtumia Gimmy International ili wakulima wapate huduma kwa wakati, na kila mdau alihusishwa, na jambo hili lilifanyika kwa nia njema,” alifafanua GM Gisiboye.

Faida ya WAMACU Serengeti
GM Gisiboye alitaja faida nyingine ambayo wakulima wa tumbaku wamepata kuwa ni uwepo wa wataalamu wa zao hilo ambao wamesaidia kuongeza ubora na kupunguza upotevu wake.

“Wataalamu wetu wamesaidia wakulima kupata bei nzuri na kuhamasisha ujenzi wa mabani ya kisasa. Juhudi hizi pia zimesaidia kuongeza ubora wa tumbaku na kuepusha upotevu wa zao hilo,” aliongeza.

Alisema Bodi ya WAMACU ina wajumbe kutoka kila wilaya, ambapo kwa wilaya ya Serengeti mjumbe wake anatokea AMCOS ya Ngarawani.

Mbali na zao la tumbaku, GM Gisiboye alisema WAMACU imepeleka mbegu na mbolea ya ruzuku katika AMCOS mbalimbali zilizopo wilayani Serengeti kama vile Machochwe, Ikorongo, Nyansurura, Kisangura na kwenye gala la Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Yajayo yanafurahisha zaidi
GM Gisiboye alisema WAMACU imejipanga vizuri kuendelea kusogeza huduma za pembejeo karibu na wakulima ili waweze kuzipata kwa umbali usiozidi kilomita 10.

Hivyo alisema yajayo kwa wakulima wa Serengeti yanafurahisha zaidi, na kuwaomba kuendelea kuwa na imani na WAMACU.

“Sio muda mrefu wakulima wa Serengeti nao wataanza kutabasumu kutokana na uwepo wa WAMACU kama ilivyo kwa wakulima wa kahawa katika wilaya za Tarime, Rorya na Butiama,” alisema GM Gisiboye.
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages