NEWS

Friday, 21 March 2025

Namibia yamuapisha Rais wake wa kwanza mwanamke, Rais Samia ampongeza



Rais mpya wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Rais mpya wa Namibia ameapishwa leo Ijumaa Machi 21, 2025 kuongoza nchi hiyo inayokabiliwa na viwango vya juu vya umaskini, ukosefu wa ajira na usawa.

Netumbo Nandi-Ndaitwah atakuwa akikabiliana na changamoto za kiuchumi sambamba na kuwa Rais mwanamke wa pili kuwahi kuchaguliwa moja kwa moja barani Afrika na Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia.

"Ikiwa mambo yataenda vizuri basi itaonekana kama mfano mzuri," Netumbo Nandi-Ndaitwah aliambia podikasti ya BBC Africa Daily.

"Lakini kama jambo lolote likitokea, kama linaweza kutokea katika utawala wowote chini ya wanaume, kuna wale ambao wangependa kusema: 'Waangalie wanawake!'

Akiwa na umri wa miaka 72, Netumbo alishinda uchaguzi kwa asilimia 57 ya kura huku mpinzani wake wa karibu Panduleni Itula akipata asilimia 26 ya kura, kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo.

Netumbo amekuwa mwanachama mwaminifu chama tawala cha SWAPO tangu akiwa msichana na kuapa kuleta mabadiliko ya kiuchumi Namibia. Alizaliwa mwaka 1952 kaskazini mwa kijiji cha Onamutai.

Ni mtoto wa tisa miongoni mwa watoto 13 na babake mzazi alikuwa kiongozi wa kidini wa Kanisa la Anglikana.

Namibia ni nchi kubwa kijiografia yenye idadi ndogo ya watu milioni tatu.

Takwimu za serikali zinaonesha kuwa wakulima wa asili ya kizungu wanamiliki takriban asilimia 70 ya mashamba ya nchi hiyo.

Jumla ya Wanamibia 53,773 waliotambuliwa kuwa wazungu katika sensa ya mwaka 2023, wakiwakilisha asilimia 1.8 ya wakazi wa nchi hiyo.

Kiwango cha ukosefu wa ajira kiliongezeka hadi asilimia 36.9 mwaka 2023 kutoka asilimia 33.4 mwaka 2018, kulingana na wakala wa takwimu nchini.

Netumbo alisema uchumi ambao kwa kiasi fulani unategemea mauzo ya madini nje ya nchi unapaswa kufanya kazi zaidi katika kuongeza thamani ya kile ambacho nchi inachimba kutoka ardhini badala ya kusafirisha malighafi nje ya nchi.

Pia, anataka Namibia kuangazia zaidi sekta za ubunifu na kufanya sekta ya elimu kuzoea hali halisi mpya ya kiuchumi.

Netumbo ni mwanamke wa pili Mwafrika kuchaguliwa moja kwa moja kama rais, baada ya Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia.

Rais mwingine mwanamke pekee wa bara hilo kwa sasa ni Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, ambaye alichukua nafasi hiyo baada ya mtangulizi wake kufariki dunia akiwa madarakani mwaka 2021.


Rais Samia akimpongeza Rais Netumbo

"Pongezi Mheshimiwa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah, kwa kuapishwa kuwa Rais wa 5 wa Jamhuri ya Namibia. Nchini Tanzania tunakujua kwa jina la Mama SWAPO, jina ulilopewa na Baba yetu Mwasisi Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Umeweka historia na kuweka kiwango cha juu kwa mtoto wa kike wa Afrika na Namibia.

"Ushindi wako mkubwa ni fahari kwa bara lakini zaidi kwa watu wa Tanzania, nyumbani kwako miaka ya nyuma. Nchini Tanzania, tunafurahi kuona binti tuliyemlea na kumkuza kwa upendo na huruma, sasa amepanda hadi ofisi kuu ya Jamhuri ya Namibia," Rais Samia ameandika leo kwenye mtandao wake wa kijamii.

Rais Samia ni miongoni mwa viongozi wa mataifa mbalimbali waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Netumbo Nandi-Ndaitwah leo.

Rais Netumbo anataka kupimwa kwa ubora wake, lakini alisema kuwa ni "jambo zuri kwamba sisi kama nchi tunatambua kwamba kama vile wanaume [wanaweza kufanya], wanawake wanaweza pia kushikilia nafasi ya mamlaka".
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages