NEWS

Saturday, 24 August 2024

AICT, Right to Play wakazia haki ya elimu kwa mtoto wa kike



Afisa Elimu Kata ya Nyamwaga, Mwalimu Gimase John akizungumza katika tamasha la michezo kwa wanafunzi, lililoandaliwa na AICT na Right to Play katani humo jana.
------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime

Shirika la Kimataifa la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe limeendelea kusisitiza kuwa elimu kwa mtoto wa kike ni muhimu kwa maendeleo ya jamii nzima.

Msisitizo huo ulitolewa wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi Maika na Nyamwaga lililoandaliwa na taasisi hizo na kufanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari JK Nyerere uliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mara jana Agosti 23, 2024.

Afisa mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Daniel Fungo alisema lengo la tamasha hilo ni kuelimisha jamii umuhimu wa wa elimu kwa mtoto wa kike katika jamii.

Fungo aliwataka watu wote kutetea haki za watoto wa kike, sambamba na kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili ili waweze kupata elimu sawa na watoto wa kiume.

Afisa mradi kutoka AICT, Daniel Fungo (kulia) akikabidhi jezi za michezo kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maika, Wajihi Baraka katika tamasha hilo.
--------------------------------------------

Kwa upande wake Afisa Elimu Kata ya Nyamwaga, Mwalimu Gimase John aliwataka wazazi na walezi kuwathamini watoto wa kike na kuhakikisha hawaachwi nyuma katika suala zima la elimu.

“Ukielimisha mtoto wa kike umeelimisha taifa, hivyo wananchi wote waliofika hapa wakawe mabalozi wa kueleza jamii kuwa mtoto wa kike sio bidhaa, waache kuwaozesha mapema, jamii iwaamini na kuwapa nafasi ya kupata elimu.

“Mashirika haya yanafanya kazi nzuri sana, waongeze bajeti kwa ajili ya kutatua changamoto za watoto wa kike. Wanaweza kufanya ubunifu kama wa kuleta taulo za kike na madaftari wakazigawa kama zawadi kwa wanafunzi,” alisema Mwalimu Gimase.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maika, Wajihi Banka alisema matamasha yanayofanyika ni jukwaa muhimu linaloleta uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.

“Matamasha haya ni mhimu sana, ni jukwaa la kuwakutanisha watoto wa jinsia zote, wananchi na viongozi kwa ajili ya kupata uelewa wa Pamoja, na hii inachangia kuondoa mtazamo hasi juu ya mtoto wa kike,” alisema Mwalimu Wajihi.

Katika tamasha hilo, wanafunzi waliweza kuonesha vipaji vyao kwa kucheza mpira wa miguu (wavula), mpira wa pete (wasichana) na kuimba ngonjera, na walipewa zawadi za jezi za kuchezea mpira na vinywaji baridi.

Tamasha hilo lilibebwa na kaulimbiu inayosema “Elimu kwa Maendeleo ya Jamii na Taifa; Toa Fursa ya Elimu kwa Mtoto wa Kike.”
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages