
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
----------------------------------------
----------------------------------------
Shirika la Kukuza Utawala Bora na Uwazi Tanzania (IGT) kwa kushirikiana na Shirika la Basis International la Uganda wamewakutanisha wadau wa sekta ya madini ya kimkakati Tanzania na kuzindua Jukwaa la Kimtandao la Kupiga Vita Rushwa kwenye Madini ya Kimkakati.
Unzinduzi huo ulifanyika jana jijini Dodoma na kuhudhuriwa na washiriki mbalimbali kutoka serikalini, mashirika yasiyo ya kiserikali, wachimbaji wadogo na wataalamu kutoka sekta ya madini.
Akifungua mkutano huo wa siku moja, Mkurugenzi wa IGT, Edwin Soko alisema jukwaa hilo linalenga kutoa nafasi kwa wadau wa sekta ya madini ya kimkakati kutumia teknolojia kwenye kuripoti taarifa mbalimbali za rushwa kwenye sekta ya madini ya kimkakati.
Madini ya kimkakati, kwa mujibu wa Soko, yana uhitaji mkubwa duniani, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuzuia biashara haramu ya madini hayo kwa kuwa yanaikosesha serikali mapato.
Jukwaa hilo litakuwa na njia mbadala katika kutoa taarifa za rushwa kwenye madini ya kimkakati yakiwemo earth rare, nickel, copper na mengineyo, hivyo hali hiyo itasaidia Taifa kupata mapato kwa maendeleo kwa Watanzania.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya Basis International, Don Binyima Bwesigye kutoka Uganda alisema ujio wa mradi huo ni utekelezaji wa azimio la ICGLR, ambapo nchi za Maziwa Makuu walikubaliana kutengeneza mfumo wa pamoja wa kuzuia rushwa kwenye sekta ya madini ya kimkakati.
Kwamba nchi hizo za Maziwa Makuu zina nafasi kuwa katika kulinda rasilimali za asili, ikiwemo madini ya kimkakati na kuketa maendeleo kwa watu wake.
Mradi huo unatekelezwa katika nchi nne za Maziwa Makuu barani Afrika; ambazo ni Tanzania, Uganda, Zambia na DRC chini ya ufadhili wa USAID Afrika.
Mtaalamu wa ICT kutoka BASIS International, Machael Mayaka aliwaeleza washiriki kuwa jukwaa hilo litawapa nafasi ya kuwasiliana katika ngazi ya kitaifa na kikanda na kujua taarifa mbalimbali za madini ya kimkakati.
Kamishina wa Tume ya Haki za Binadamu, Thomas Masanja alieleza nafasi ya tume hiyo kwenye kupokea malalamiko, yakiwemo ya sekta ya madini akisema jukwaa hilo litazidi kuimarisha ushirikiano.
Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka (DPP), Renatus Mkude alisema ofisi yake inatafuta ushahidi kwa kujiridhisha kabla ya kuchukua hatua za kufungua mashtaka zikiwemo kesi za madini ya kimkakati.
No comments:
Post a Comment