Sehemu ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Mara wakishiriki mafunzo.
----------------------------------------
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wametakiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura muda wote hata kama hakuna waombaji wa kujiandikisha vituoni.
Wito huo ulitolewa mjini Musoma jana na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele wakati akifunga mafunzo kwa watendaji wa uboreshaji wa daftari hilo ngazi ya halmashauri na mkoa wa Mara.
Alisema watendaji wa vituo wanapaswa kuwepo vituoni muda wote kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kila siku katika siku saba za kujiandikisha zilizowekwa na INEC.
“Muda wa kufungua na kufunga kituo uwe ni ule uliopangwa ili waombaji wanapohitaji kuja kituoni kujiandikisha watukute kituoni,” alisisitiza Jaji Mwambegele.
Jaji Mwambegele akifungua
mafunzo hayo mkoani Mara.
-------------------------------------
Tukio kama hilo la kufunga mafunzo lilifanyika pia mkoani Simiyu ambako Mjumbe wa INEC, Magdalena Rwebangwira aliwataka watendaji hao kufuatilia kwa karibu shughuli hiyo ili ifanikiwe, kutoa kipaumbele kwa makundi mbalimbali na kuwa makini katika usambazaji na utunzaji wa vifaa.
Akifunga mafunzo ya watendaji mkoani Manyara, Mjumbe wa INEC ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari kwa upande wake alihimiza uhamasishaji wa wapiga kura na kuwa Tume inatarajia wapiga kura halali tu ndio wapatiwe kadi za mpiga kura.
“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki kuwachagua viongozi wao. Aidha ni matarajio ya Tume kuwa baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaopatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali,” alisema Jaji Asina.
Mafunzo kwa vitendo
-----------------------------
Mafunzo hayo ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mzunguko wa nne unaojumuisha mikoa ya Mara na Simiyu, na baadhi ya halmashauri za mkoa wa Manyara; ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu, ambapo uboreshaji utaanza Septemba 4 hadi Septemba 10, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>> MNEC Boghohe awasili Tarime kumwakilisha Mwenyekiti UWT CCM Taifa harambee ya kuchangia vitega uchumi vya UWT
>> Nyangwine ameonesha uzalendo kutangaza bidhaa, vivutio vya utalii vya Tanzania kimataifa
>>Tanzanian medico elected WHO Africa Regional Director
>> Mtanzania Dkt Faustine Ndugulile achaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika
No comments:
Post a Comment