NEWS

Wednesday, 28 August 2024

Nyangwine ameonesha uzalendo kutangaza bidhaa, vivutio vya utalii vya Tanzania kimataifa



Nyambari Nyangwine
-----------------------------

Na Christopher Gamaina
chrisgapressman@gmail.com

Katika siku za karibuni, Tanzania imeshuhudia juhudi za kipekee kutoka kwa mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine ambaye amejitolea kwa dhati kuunga mkono juhudi za serikali katika kuitangaza nchi yetu kimataifa.

Nyangwine ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara kwa tiketi ya chama tawala - CCM, ameonesha juhudi za dhati katika kutangaza bidhaa mbalimbali na vivutio vya utalii vya Tanzania katika mataifa ya nje.

Kupitia biashara zake, uhusiano na ushirikiano wake na wafanyabiashara, mashirika na kampuni za kimataifa, Nyangwine amekuwa nyenzo muhimu katika kuvutia uwekezaji wa kigeni na kukuza utalii kwa Tanzania.

Mfano hivi karibuni, Nyangwine alifanya ziara ya kibiashara ya siku saba katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambako alitembelea miji mbalimbali na kukutana na watu tofauti katika nchi za Dubai, Abu Dhabi na Sharjah.

Akiwa amefuatana na msafara wa watu sita, Nyangwine alitumia fursa hiyo kutangaza bidhaa mbalimbali za Tanzania kwenye masoko ya UAE. Bidhaa hizo ni pamoja na kahawa, asali, majani ya chai na korosho zinazozalishwa Tanzania.

Kabla ya UAE, Nyangwine alifanya ziara ya kibiashara ya wiki moja nchini India, ambapo pia pamoja na ratiba nyingine, alikutana na Waziri wa Utalii wa India, Shri Gajendra Singh Shekhawat na kumpatia zawadi ya bidhaa tofauti kutoka Tanzania, yakiwemo majarida mbalimbali yanayoonesha vivutio vya utalii vilivyopo kwenye hifadhi za wanyamapori hapa nchini.

Nyambari Nyangwine (mwenye kofia) akimkabidhi Waziri wa Utalii wa India, Shri Gajendra Singh Shekhawat zawadi ya bidhaa mbalimbali za Tanzania, Jijini New Delhi, India, hivi karibuni.
----------------------------------------------

Lakini pia, Nyangwine aliweza kukutana na wafanyabiashara mbalimbali na wadau wa utalii katika mataifa hayo ya nje kuzungumzia uzinduzi wa Nyambari Nyangwine Foundation utakaofanyika jijini Dar es Salaam. Septemba mwaka huu.

Nyangwine ameweza kutumia ziara hizo za ughaibuni kuwafahamisha wawekezaji na watalii kuhusu fursa za kipekee zilizopo Tanzania.

Kwa kushirikiana na marafiki na wafanyabiashara wenzake, Nyangwine amethubutu kutangaza bidhaa za Tanzania ili ziweze kupata nafasi nzuri kwenye soko la kimataifa. Hatua hii inachangia kuimarisha mtandao wa uhusiano wa kibiashara na wenye matumaini ya kuleta matokeo chanya kwa sekta ya utalii nchini.

Kupitia juhudi hizi za Nyangwine, bidhaa na vivutio vya utalii vya Tanzania vinapata umaarufu na soko kubwa katika nchi anazotembelea.

Kutangaza bidhaa na vivutio vya utalii vya Tanzania kama anavyofanya Nyangwine kunasaidia kuvutia wageni kutoka nchi nyingine. Wageni hao wanapokuja nchini wanachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi kupitia matumizi yao katika maeneo ya utalii, hoteli na huduma nyingine.

Kukuza picha ya Tanzania kama eneo la kuvutia wawekezaji wa kigeni kunaweza kuongeza mtiririko wa uwekezaji. Miradi ya maendeleo, viwanda na huduma mbalimbali zitapata rasilimali za kuimarisha uchumi wa taifa letu.

Ongezeko la watalii na wawekezaji linachangia katika kutengeneza ajira mpya. Sekta ya utalii ni muhimu sana katika kutoa ajira, na hivyo kuongeza fursa za kazi kwa wananchi.

Kuimarisha sekta ya utalii kuna umuhimu mkubwa katika uhifadhi wa maeneo ya kihistoria, maliasili na mazingira. Hii ni muhimu kwa ajili ya kudumisha urithi wa kitaifa na mazingira safi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Nyangwine ameonesha mfano mzuri wa jinsi mfanyabiashara wa Kitanzania anavyoweza kuchangia kwenye maendeleo ya taifa kwa kujitolea kutangaza bidhaa na vivutio vya utalii.

Juhudi hizi za Nyangwine zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza picha ya Tanzania kimataifa, kuvutia wageni, kuongeza uwekezaji na kuimarisha uchumi wa taifa letu.

Ni muhimu kwa wafanyabiashara, wanasiasa na wananchi wengine kuiga mfano huu wa Nyangwine wa kujitolea ili kuchochea maendeleo chanya ya biashara na utalii, miongoni mwa sekta nyingine Tanzania.

Heko Nyambari Nyangwine kwa kudhihirisha uzalendo wako na dhamira ya kujitolea katika kutangaza bidhaa na vivutio vya utalii vya Tanzania kwa manufaa ya Watanzania.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages