NEWS

Wednesday, 28 August 2024

Mtanzania Dkt Faustine Ndugulile achaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika

                  Dkt Faustine Ndugulile (katikati mwenye shati jeupe)
        --------------------------

Dkt Faustine Ndugulile wa Tanzania amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.

Dkt Ndugulile, mtaalam wa afya ya umma ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam alikuwa mmoja wa wagombea watano waliojitokeza kurithi mikoba ya Dk Matshidiso Moeti.

Dkt Moeti, raia wa Botswana anatarajiwa kuhitimisha muhula wake wa pili kama Mkurugenzi wa Kanda wa WHO katika kikao cha 74 kinachoendelea cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO huko nchini Congo Brazzaville tangu Agosti 26 hadi Agosti 30, 2024.

Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan alituma pongezi zake za dhati kwa Dkt Ndugulile kwa kuchaguliwa akisema, “Umeifanya nchi yetu kuwa na fahari, na bara letu litafaidika sana na kazi yako.”

Rais Samia alisema kwenye 'X' jana Jumanne, "Nina imani kwamba ujuzi wako na uzoefu wako katika sekta ya afya utaiwezesha Afrika kuwa na sauti muhimu katika ngazi ya kimataifa katika kukabiliana na changamoto za afya kwa mamilioni ya watu wetu katika bara."

Mtanzania huyo alikuwa akishindana na Dkt Boureima Hama Sambo wa Niger, Dkt Richard Mihigo wa Rwanda, Dkt N’da Konan Michel Ya wa Ivory Coast na Dkt Ibrahima Socé Fall wa Senegal.

Taaluma na kazi:

Dkt Ndugulile ni Daktari Tiba na ana Shahada ya Uzamili ya Tiba katika Tiba Mikrobiolojia na Kinga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya Uzamili ya Afya ya Umma (MPH) kutoka Chuo Kikuu cha Western Cape, na Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) kutoka Open University of Tanzania (Chuo Kikuu Huria cha Tanzania).

Pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya ya Bunge la Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kimataifa (IPU) Advisory Group Health na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mtandao wa Kamati za Afya za Bunge la Afrika (NEAPACOH).

Dkt Ndugulile aliwahi kuwa naibu waziri wa Afya wa Tanzania kati ya 2017-2020, pia aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari 2020-2021.

Pia amefanya kazi kama mkurugenzi katika Wizara ya Afya Tanzania anayeshughulikia huduma za uchunguzi na pia meneja wa programu mwanzilishi wa Huduma ya Kitaifa ya Usambazaji Damu mwaka 2006.

Kati ya 2007-2010, aliwahi kuwa Mshauri Mkazi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) nchini Afrika Kusini akitoa msaada wa kiufundi kwa nchi nyingine nyingi kama vile Angola, Msumbiji, Tanzania na Rwanda.

CHANZO:BBC

Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages