NEWS

Thursday, 29 August 2024

Jubilei ya Askofu Msonganzila: Rais Samia achangia Kanisa milioni 30/-



Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Mhashamu Michael Msonganzila akibariki matoleo ya waamini wakati wa maadhimisho ya Jubilei yake ya Miaka 40 ya Upadre, leo Agosti 29, 2024.
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa mchango wa shilingi milioni 30 kwa ajili ya shughuli za kiroho za Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma.

Fedha hizo zimewasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi ambaye amemwakilisha Rais Samia katika Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre ya Mhashamu Michael Msonganzila, Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma.

Sherehe hizo ambazo zimefana kwa aina yake, zimefanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma, Mara leo Agosti 29, 2024.

Akiwasilisha ujumbe wa Rais Samia, Waziri Ndejembi amesema serikali inatambua na kuthamini mchango wa viongozi wa dini katika kujenga amani, umoja, upendo na kuliombea taifa, hivyo itaendelea kushirikiana nao kwa maendeleo ya Watanzania.

Sherehe hizo pia zimehudhuriwa na viongozi wengine mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na dini, akiwemo Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Kadinali Polycarp Pengo.


Askofu Msonganzila katika picha ya pamoja na Maaskofu mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo.
----------------------------------------

Kadinali Pengo amempongeza Askofu Msonganzila, na kutumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha waamini kumkumbuka Mungu kwa shukrani.

“Ikiwa furaha yako inakufanya usahau kwenda kusema asante kwa Mwenyezi Mungu, hiyo furaha ina tatizo,” amesema Kadinali Pengo na kuendelea:

“Tumeitikia mwaliko wako Askofu Msonganzila leo, ni nafasi ya sisi kutafakari ukuu wa Mungu na kusema asante, miaka 40 ni safari ndefu. Wewe umekuwa dira kwa kusaidia mabinti pa kukimbilia wapate faraja, ukishirikiana Graca Machel, huduma inaonesha ulivyomtangaza Kristo kwa watu kwa miaka 40 ya upadre wako.”

Kwa upande wake Askofu Msongazila ambaye amefikisha umri wa miaka 68 tangu kuzaliwa, ametoa neno la shukrani kwa Rais Samia na makundi ya watu alioshirikiana nao katika shughuli za kiroho.

“Ninawashukuru wote; maaskofu, mapadre, watawa, makatekista na wote ambao sikuwataja, asanteni. Pia namshukuru Mama Samia Suluhu Hassan, naahidi kwa sala aweze kuongoza vema nchi hii,” amesema Askofu Msonganzila.


Pamoja na zawadi nyingine kutoka kwa makundi mbalimbali, Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma limekabidhi hundi ya shilingi milioni 100 wakati wa sherehe hizo za Jumbilei ya Miaka 40 ya Upadre ya Askofu Msonganzila.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages