
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
----------------------------------------------
Msako wa mara na doria zinazoendeshwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga vimefanikisha kutiwa mbaroni kwa watu kadhaa wanaojihusisha na biashara haramu ya mirungi na usafirishaji madini kinyume cha sheria.
Katika msako huo, mtu mmoja alikamatwa akiwa na mirungi yenye uzito wa gramu 400 aliyokuwa akisafirisha kwenye gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T 886 DCU linalofanya safari kati ya Shinyanga na Kahama.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, tangu Julai 25 mwaka huu, jeshi hilo limekuwa likiendesha msako uliofanikiwa kuwanasa wahalifu katika maeneo ya Nyakato, manispaa ya Kahama.
Kamanda Magomi amewambia waandishi wa habari ofisini kwake leo kwamba katika tukio hilo watu wawili walikamatwa wakiwa na madini ya dhahabu vipande vitatu vilivyochomwa vyenye uzito wa gramu 13.35, mzani na fedha taslimu shilingi 2,799,000.
Pia, Agosti 1, 2024, watu wengine wanne walikamatwa eneo la Nyasubi, manispaa ya Kahama, wakiwa na vipande 11 vyenye uzito wa gramu 652.6 vya madini yanayodhaniwa kuwa dhahabu.
Watuhumiwa hao, ambao tayari wameshafikishwa mahakamani, pia walikutwa wakiwa na gari aina ya Suzuki Vitara, fedha taslimu shilingi milioni 96, pikipiki sita, vipande 12 vya nondo, magodoro mawili, redio tatu, simu nne na pipa la kuchenjulia dhahabu.
No comments:
Post a Comment