Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akikata utepe kabla ya kukabidhi pikipiki zilizotolewa na RUWASA Wilaya ya Tarime kwa ajili ya viongozi wa vyombo vya huduma ya maji ngazi ya jamii leo Oktoba 22, 2024.
-------------------------------------------
Tarime
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Meja Edward Gowele amewaelekeza viongozi wa vyombo vya huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSOS) kutumia pikipiki walizopewa na RUWASA kwa kazi zilizokusudiwa.
Meja Gowele ametoa maelekezo hayo wakati akikabidhi pikipiki saba kwa viongozi wa vyombo hivyo katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi za Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime leo Oktoba 22, 2024.
“Katumieni vyombo hivi vya usafiri katika shughuli za kutatua changamoto za maji kwa wananchi. Msizitumie kufanya magendo na shughuli za bodaboda (kusafirisha abiria),” amesisitiza DC huyo na kutahadharisha kuwa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watakaozitumia vibaya.
Aidha, ameielekeza RUWASA kufuatilia mienendo wa matumizi ya pikipiki hizo ili kuhakikisha zinatumika vizuri, wakitambua kuwa zimenunuliwa kutokana na kodi za wananchi.
Meja Gowele ametumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha utoaji wa fedha zilizotumika kununua pikipiki hizo kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Awali, mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Pasian Martin amemueleza Meja Gowele kuwa ofisi yao imetumia shilingi milioni 21 kununua pikipiki hizo, na kwamba wilaya hiyo ina CBWSOS saba.
Amezitaja CBWSOS hizo zenye jukumu la kusimamia uendelevu wa miradi ya maji kuwa ni Sirari, Nyamongo, Ingwe, Inchage, Kiribo, Keisangura-Nyamwaga na Nyandoto-Kenyamanyori.
“RUWASA inavisimamia vyombo hivi kwa kuvipa msaada wa kiufundi na vitendea kazi ili kuboresha huduma za maji kwa wananchi,” amesema Mhandisi Martin na kumshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha sekta ya maji na kumtua mama ndoo ya maji kichwani.
Kwa upande wao viongozi wa CBWSOS waliopewa pikipiki hizo wameishukuru RUWASA na serikali kwa ujumla wakisema zitawasaidia kuongeza ufanisi wa kazi.
“Ninashukuru sana, pikipiki hizi zitatuwezesha kuwafikia watumia maji na kuwatatulia changamoto kwa wakati,” amesema Jean Mwita Manga, Mwenyekiti wa CBWSO ya Sirari.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Shirika la MYCN lawataka vijana kuwa mabalozi wa utunzaji mazingira kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
>>Mwenyekiti CCM Mara awapongeza wanachama kwa uchaguzi wa amani
>>Rock City Malls yawa kivutio cha utalii jijini Mwanza
>>Serengeti, Mlima Kilimanjaro zaendelea kuiheshimisha Tanzania kimataifa
No comments:
Post a Comment