NEWS

Sunday, 20 October 2024

Serengeti, Mlima Kilimanjaro zaendelea kuiheshimisha Tanzania kimataifa

Tuzo zilizotolewa
---------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Taasisi ya World Travel Awards imezitangaza Hifadhi za Taifa Serengeti na Mlima Kilimanjaro za Tanzania kushinda tuzo za ubora barani Afrika kwa mwaka 2024.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Ijumaa iliyopita, Hifadhi ya Taifa Serengeti imetangazwa kushinda Tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika (Africa’s Leading National Park 2024).


Nayo Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro imetangazwa kushinda Tuzo ya Kivutio Bora cha Utalii (African Leading Tourist Attraction 2024).

Tuzo hizo zilitolewa Oktoba 18, mwaka huu usiku katika ukumbi wa Hoteli ya Diamonds Leisure Beach & Golf Resort, Nairobi nchini Kenya.

Mwanzilishi wa Taasisi ya World Travel Awards, Graham Cooke alisema Serengeti imezishinda hifadhi za Maasai Mara ya Kenya, Kruger (Afrika Kusini), Central Kalahari (Botswana), Etosha (Namibia) na Kidepo Valley (Uganda).

Kwa upande wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, alisema imevishinda vivutio vingine vya utalii Afrika ambavyo ni hifadhi za Ngorongoro (Tanzania), Hartbeespoort Aerial Cableway, V & A, Waterfront, Robben Island na Table Mountain (Afrika Kusini), Ziwa Malawi, Okavango Delta (Botswana) na Pyramid ya Misri.


Tuzo hizo zilipokewa na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu anyashughulikia utalii, Nkoba Mabula, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii, Ephraim Mafuru, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, CPA Hadija Ramadhani, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Betrita Lyimo na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi.

Kwa ushindi huo, Hifadhi ya Taifa Serengeti imeweka rekodi ya kushinda Tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika kwa mara ya sita mfululizo (mwaka 2019 hadi 2024).

Ushindi wa mwaka huu pamoja na jitihada zingine, umechagizwa na kampeni ya TANAPA ya “Vote Now” iliyofanyika kwa miezi mitatu mfululizo, kwa mujibu wa TANAPA.

“Kwa upande wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro imeshinda Tuzo ya Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika mwaka 2013, 2015, 2016, 2017, 2018 na 2024, ikiwa ni mara ya sita,” ilieleza taarifa hiyo ya TANAPA iliyosainiwa na Afisa Uhifadhi Mkuu Kitengo Mawasiliano, Catherine Mbena.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages