
Safari ya matembezi ya kilomita 284 ya vijana wa UVCCM Mkoa wa Mara imeanza leo kuelekea mkoani Mwanza.
------------------------------------------

Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi Omary (aliyevaa skafu) akiongozana na akiwasili wilayani Butiama kuzindua matembezi ya vijana mapema leo. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Umoja huo Mkoa wa Mara, Mary Daniel Joseph. (Picha na Mara Online News)
-----------------------------------
Butiama
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Rehema Sombi Omary amezindua matembezi ya kilomita 284 ya wanachama wa umoja huo kutoka mkoani Mara kwenda jijini Mwanza.
Matembezi hayo ambayo yanaanzia wilayani Butiama yatapokewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza wakati wa kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Oktoba 14, 2024.
Lengo la matembezi hayo ambayo yanawashirikisha wana-UVCCM zaidi ya 1,500 ni kuenzi kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mzaliwa wa Butiama.

Makamu Mwenyekiti Rehema Sombi akivishwa skafu na mmoja wa wanachama wa UVCCM Mkoa wa Mara.
-------------------------------------
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa matembezi hayo leo, Makamu Mwenyekiti Rehema Sombi ambaye ameambatana na Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Jokate Mwegelo, aliwataka wanachama wa umaja huo kulinda tunu za taifa.
"UVCCM tunao wajibu wa kulinda na kutunza tunu za taifa, ikiwemo lugha ya Taifa ya Kiswahili, amani, mapinduzi matukufu ya Zanzibar, Muungano na Mwenge wa Uhuru -maana historia yake inaonesha mchango wa Baba Taifa," amesema.
Aidha, Rehema Sombi amewataka kutumia nafasi ya matembezi hayo kuhamasisha vijana wenzao umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika nchini Novemba 27, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment