Viongozi wakikabidhi zawadi ya jezi kwa wanafunzi wakati wa tamasha la michezo lililoandaliwa na Kanisa la AICT na Shirika la Right to Play katika Shule ya Msingi Tumaini wilayani Serengeti juzi Oktoba29, 2024. Picha na Mara Online News)
-------------------------------------------
Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play wameadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani kwa kuhamasisha jamii kuwapatia watoto wa kike haki ya kupata elimu.
Uhamasishaji huo ulifanyika juzi Oktoba 29, 2024 wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi lililoandaliwa na taasisi hizo katika Shule ya Msingi Tumaini iliyopo wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Afisa Mradi wa Save Her Seat na Elimu Jumuishi kutoka AICT na Right to Play, Daniel Fungo alitoa wito wa kuhamasisha kila mmoja kuwa balozi wa kupiga vita vikwazo vya elimu kwa watoto wa kike.
"Tuwe mabalozi wa kutokomeza vitendo vinavyokwamisha mtoto wa kike kupata elimu. Watoto wa kike wakisoma wanasaidia kuliko wa kiume, hivyo wapatiwe fursa kusoma kama wa kiume," alisisitiza Fungo.
Mwanafunzi wa shule hiyo, Evaline Samson aliishukuru AICT na Right to Play kwa kuwapa elimu ya stadi za maisha kupitia mradi wa Save Her Seat.

Evaline Samson
----------------------
"Nimezielewa haki zangu, haki za mtoto za kuishi, kulindwa, kuendelezwa na kushirikishwa mambo yanayotuhusu watoto wa kike katika jamii," alisema Evaline.
Alisema wazazi kutozungumza na watoto ni changamoto kubwa. "Moja ya changamoto inayotukabili ni wazazi kukosa muda wa kuzungumza na sisi ili kujua changamoto tunazopitia," alisema.

Mwalimu Gladis Magati
-------------------------------
Naye Mwalimu Mlezi wa Klabu ya Mradi wa Save Her Seat katika Shule ya Msingi Tumaini, Gladis Magati alisema kwamba kupitia mradi huo wameweza kuwafundisha wanafunzi stadi za maisha, hivyo kuwajengea wanafunzi hali ya kujiamini na kuimarisha mahusiano mema baina yao.
Tamasha hilo lilihusisha michezo ya mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa pete kwa wasichana, kukimbia kwenye gunia, ngonera, maigizo na kukimbia na chupa kichwani. Washindi walizawadiwa jezi na vinywaji baridi.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>HABARI PICHA:Viongozi wamiminika kuagwa kwa mwili wa Jenerali Musuguri Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo
>>Profesa Kithure Kindiki aapishwa rasmi kuwa Naibu Rais mpya wa Kenya, amshukuru Rais Ruto, amuahidi utiifu
>>Gachagua apata pigo tena, jaribio lake la kuzuia kuapishwa kwa Kindiki kuwa Naibu Rais wa Kenya lagonga mwamba
>>NECTA yatangaza matokeo ya darasa la saba 2024
No comments:
Post a Comment