
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza katika kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma juzi.
---------------------------------------
Mitambo 25 ya kisasa iliyotumika kuchimba visima 650 katika vijiji 876 nchini imeleta mapinduzi makubwa kwa kuwezesha wananchi zaidi ya milioni sita kupata majisafi na salama.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dodoma jana na Wizara ya Maji kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jackson Kiswaga ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, ilieleza kwamba visima hivyo vimechimbwa kwa kutumia mitambo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.

Majadiliano yakiendelea katika kikao hicho mjini Dodoma.
---------------------------------------
Rais Samia alitoa mitambo hiyo ili kuimarisha huduma ya majisafi na salama nchini ili kukidhi mahitaji ya mamilioni ya Watanzania waishio vijijini.
Taarifa hiyo pia imegusia hatua iliyofikiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika usambazaji wa maji ya visima.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mitambo hiyo ya teknolojia ya kisasa inajenga weledi na ufanisi kwa wataalamu na watendaji wengine katika kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini.
Azma ya Serikali ya Tanzania ni kuhaikikisha kwamba wananchi wanaoishi vijijini wanapata huduma bora na endelevu ya majisafi na salama kwa asilimia 85 ifikapo mwakani 2025, wakati waishio mijini wanapata huduma hiyo kwa asilimia 95.
No comments:
Post a Comment