NEWS

Sunday, 20 October 2024

Nyambari Nyangwine awapa vijana misingi ya kujenga taifa akihutubia mahafali ya kidato cha nne Mbezi High School



Nyambari Nyangwine akikabidhi vyeti kwa wahitimu wakati wa Mahafali ya 22 ya Kidato cha Nne ya Sekondari ya Mbezi High School jijini Dae es Salaam juzi.
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine amewakumbusha vijana wa Tanzania kujikita kwenye misingi inayoweza kuwaletea mafanikio ya kimaisha na kujenga taifa lenye maendeleo ya kisekta.

Amesisitiza umuhimu wa vijana wa leo kuwa wakweli, wawazi, na wachapakazi, huku wakionesha ubunifu na uthubutu katika kufikia malengo yao.

Akihutubia umati wa watu katika Mahafali ya 22 ya Kidato cha Nne ya Sekondari ya Mbezi High School jijini Dar es Salaam juzi, Nyambari aliongeza kwamba vijana pia wanapaswa kuwa na upendo, utii, hekima, uzalendo na misimamo thabiti - kama nguzo muhimu katika kujenga taifa lenye nguvu na maono.

“Vile vile kijana wa leo anapaswa kuwa msikivu, mnyenyekevu, hodari na jasiri katika kukabiliana na changamoto na mwenye maono na uzalendo wa kweli kwa nchi yake,” aliongeza Nyambari katika hotuba yake iliyotia moyo na hamasa kubwa kwa vijana.

Aidha, Nyambari ambaye pia ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Group of Companies Ltd, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Foundation (NNF), alisema ni muhimu pia kwa kijana kujua alipotoka, alipo na anapotaka kwenda.

Kuhusu elimu kwa vijana wa Tanzania na Afrika, alisema ni vizuri itumike katika kubadili mitazamo kiakili, kiimani, kimalengo, kitabia, kimatendo na kimazingira.

“Elimu iwe ukombozi wa kweli wa kifikra,” alisema aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara kupitia chama tawala - CCM.

“Vijana wanapaswa kutumia elimu yao vizuri katika kusimamia ukweli, wautafute ukweli, wauishi ukweli, waulinde, wautetee na kupigania ukweli na kupinga uongo wa aina yoyote.

“Stadi za maisha zinapaswa kuwasaidia vijana kujiajiri na sio kukimbilia kuajiriwa. Elimu na mazingira viwe msaada kwa vijana kuyatawala na kuyamiliki mazingira yanayowazunguka,” alisema Nyambari.

Alizidi kusisitiza kuwa elimu inapaswa kuwasaidia vijana kujibu masuala kwa kutumia tafiti na si kwa vioja visivyo na msingi. “Changamoto za vijana zinapaswa kutatuliwa na vijana wenyewe kwa kushirikishwa katika majadiliano, na siyo kudanganywa kuwa wao ndio viongozi wa kesho,” alisema.

Aliendelea: “Kumbuka linalowezekana leo halipaswi kusubiri kesho. Ni muhimu pia kukumbuka kwamba vijana ndio waliofanya mambo makubwa duniani, hasa katika mageuzi ya kiuchumi, sayansi na teknolojia.”


Nyambari Nyangwine akiendelea kukabidhi vyeti kwa wahitimu wa kidato cha nne.
---------------------------------------

Nyambari alisema vijana wa sasa wanatakiwa kujifunza kujadili masuala na si watu. “Mawazo madogo hujadili watu, mawazo ya wastani hujadili matukio na mawazo makubwa hujadili hoja. Kila kijana anapaswa kuwa mtulivu, kufanya utafiti wa kutosha na kuepuka kufuata mkumbo,” alisisitiza.

“Ni muhimu kujua kuwa kufikiri kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili ndiyo matumizi bora ya akili. Hii itawasaidia vijana kujiamini na kuwa na nguvu katika kutumikia jamii zao,” alisema.

Aliongeza kuwa kijana wa Kitanzania na Afrika anapaswa kutumia vipawa alivyonavyo kutatua changamoto za umaskini, elimu, afya na ajira pamoja na kupiga vita vitendo vya rushwa na kutetea haki zao bila hofu.

Sambamba na hayo, Nyambari alisema vijana wa Tanzania na Afrika kwa ujumla wanapaswa kuepuka kabisa akili ya kuchomekewa, badala yake wawe watu wa kujiongeza kwa kila hatua ya maisha ili kuleta ufanisi katika maisha yao.

“Pia, vijana wa Tanzania wanatakiwa kutambua na kulinda rasilimali muhimu za taifa lao. Wasitumie nafasi walizonazo kuzipora rasilimali hizo. Kwa ufupi, tamaa ya utajiri wa haraka haraka hauna mustakabali mzuri kwa taifa letu,” Nyambari alionya.

“Vijana wa Tanzania wanatakiwa wawe msaada kwa wengine, hasa maskini wasio na uhakika wa mlo wao wa leo au kesho, kwa kuwasaidia kwa juhudi na maarifa. Ikiwa huwezi kuwasaidia, basi usiwaumize kwa kupora rasilimali zao, au kupokea rushwa, au kuwafitini katika mamlaka mbalimbali.

“Vijana wa Tanzania na Afrika hawapaswi kukata tamaa katika juhudi zao za kupambana na maisha. Maneno kama “MCHIZI WANGU IPO SIKU NITATOBOA” bila kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

“Vijana wa Tanzania wanapaswa kujifunza lugha mbalimbali za kigeni ili waweze kuwasiliana na vijana wengine duniani, kwani Tanzania siyo kisiwa,” alisisitiza Nyambari.

Kuhusu mitandao ya kijamii, alisema ni muhimu itumike kwa manufaa na siyo kwa uhalifu, au kulalamika. “Vijana wanapaswa kujihadhari na mambo yasiyofaa kama ushoga na usagaji,” alisema.

Aliongeza: “Nidhamu isiyo na uoga ni muhimu kwa vijana ili kuhoji masuala yanayowahusu na nchi zao. Wathubutu kugombea nafasi za uongozi.

“Vijana wa Tanzania wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli kwa nchi yao. Wapigie debe nchi yao kwa dhati, kwani hiyo ndiyo nchi waliyopewa na Mwenyezi Mungu, na hakuna nchi nyingine. Ushirikiano ni muhimu, kwani umoja ni nguvu. Waepuke ubinafsi kwani kidole kimoja hakivunji chawa.

“Vijana wa Tanzania na Afrika wanapaswa kuepuka vitendo viovu kama uvutaji bangi, matumizi ya dawa za kulevya, umalaya, wizi, na ujambazi. Badala yake, watumie muda wao kujifunza na kujiongezea maarifa,” alisema Nyambari Nyangwine.

“Mwisho, vijana wa Tanzania nawasisitizia kuwa mshikeni elimu, hata katika vitabu vya dini vimeandika kuhusu umuhimu wa elimu kwani ndiyo mkombozi wetu. Elimu, elimu, elimu, elimu ndiyo silaha pekee inayoweza kuleta mapinduzi ya kifikra katika bara la Afrika,” alisisitiza.


Nyambari Nyangwine (aliyevaa kofia) akiwa na uongozi wa Sekondari ya Mbezi High School jijini Dar es Salaam alipowasili kwa ajili ya kushiriki kama mgeni rasmi katika Mahafali ya 22 ya Kidato cha Nne jyzu.
----------------------------------------------

Kuhusu changamoto zilizorodheshwa katika risala ya wanafunzi na hotuba ya Mkuu wa Sekondari ya Mbezi High School, ikiwemo upungufu wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia, Nyambari Nyangwine Group of Companies Ltd kupitia taasisi yake ya Nyambari Nyangwine Foundation iliipatia shule hito msaada wa vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni 10.240.

“Vitabu hivi vitasaidia kuziba pengo lilopo na kuboresha mazingira ya kujifunzia, vitakuwa nyenzo muhimu katika kukuza elimu na vitawawezesha wanafunzi wetu kuweza kujifunza na kufahamu kwa kina masomo yao,” alisema Nyambari.

Pia, Nyambari Nyangwine Group kupitia NNF iliipatia shule hiyo msaada wa vifaa vya michezo, ikiwemo mipira ya soka, pete, kikapu na volleyball vyenye thamani ya shilingi 480,000.

“Hivi vifaa vya michezo vitasaidia kuimarisha michezo katika shule na kukuza talanta za wanafunzi wetu katika michezo na kuwapa fursa ya kujenga afya zao. Michezo inasaidia pia katika kukuza uhusiano mzuri kati ya wanafunzi na kujenga umoja shuleni,” alisema Nyambari.

Lakini pia, Nyambari Nyangwine Group kupitia Taasisi yake ya Nyambari Nyangwine Foundation aliipatia shule hiyo msaada wa saa nne za ukutani zenye thamani ya shilingi 200,000. “Saa hizi zitasaidia wanafunzi kujifunza jinsi ya kutumia muda vizuri katika masomo yao,” alisema.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages