![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi( mwenye kofia kulia) akiteta na wakazi wa Butiama jana kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ujayo( picha na ofisi ya RC Mara) |
Na Mwandishi Wetu
Wananchi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara wamehimizwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu katika azima ya taifa ya kujenga utawala bora.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alipotembelea Wilaya ya Butiama kukagua maendeleo ya uandikishaji wapiga kura na hali ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa.
Alisema kujiandikisha pekee kama mpiga kura hakutoshi bila ya wananchi wenyewe kushiriki katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi ya kitongoji, kijiji na udiwani.
“Tuitumie fursa hii ya kikatiba vizuri ili kuwachagua viongozi wanaofaa ili waweze kusimamia miradi ya maendeleo na kushughulikia kero zetu katika maeneo yetu,” Kanali Mtambi alisema.
Aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na kwamba iwapo kuna changamoto wazishughulikie mara moja ili uchaguzi uwe huru na wa haki.
Mkazi wa kitongoji cha Kitanga, Kijiji cha Butiama, Nassoro Swaibu, alimpongeza Kanali Mtambi kwa kukitembelea kitongoji hicho kwa ajili ya kuwahamasisha kuwachagua viongozi bora.
Naye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Butiama, Gosbert Bernard, alisema jimbo hilo linategemea kuandikisha wapiga kura 183,855 na kwamba hadi Jumatatu Oktoba 14, 2024, idadi ya wananchi waliojiandikisha ilifikia watu 53,048, sawa na asilimia 38.8.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa lilianza Oktoba 11, 2024 na linatarajiwa kukamilika Oktoba 20.
No comments:
Post a Comment