
NA MWANDISHI WETU, Musoma
---------------------------------------------
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imefanikiwa kunusuru wizi wa mabati 104 yenye thamani ya shilingi milioni 4.576 katika wilaya ya Serengeti.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Musoma wiki iliyopita, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff alosema mabati hayo ni ya mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Chifu Sarota iliyopo kata ya Nagusi, Serengeti.
“Ufuatiliaji ulibaini kuwa mzabuni alipaswa kuwasilisha mabati 800 kwa mujibu wa makubaliano, lakini aliwasilisha mabati 696 baada ya kula njama ya kuiba mabati ambayo hakuyawasilisha, kwa kushirikiana na msimamizi wa mradi huo,” Shariff alisema.
Kwa upande mwingine, TAKUKURU kupitia programu yake ya TAKUKURU Rafiki, imesaidia kulipwa kwa deni sugu la shilingi 37,500,000 ambazo ni kwa ajili ya kugharimia shughuli za utawala kutokana na makubaliano baina ya Serikali ya Kijiji cha Seka kilichopo kata ya Nyamrandirira, wilaya ya Musoma na Kampuni ya MMG GOLD Ltd kwa ajili ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).
Aidha, Shariff alisema TAKUKURU imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 32 yenye thamaniya shilingi bilioni 43.55 katika sekta za afya, elimu, barabara na maji.
“Kati ya miradi hiyo 32, minne yenye thamani ya shilingi milioni 655 ilikuwa na dosari, na hatua zilizochukuliwa zimekuwa na mafanikio,” alisema.
Hata hivyo, alisema ofisi yake imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya masuala ya rushwa inaenezwa katika taasisi za serikali, binafsi na wananchi ili kuongeza wigo wa mapambano dhidi ya rushwa.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Uchaguzi Serikali za Mitaa: Lissu kuzindua kampeni za CHADEMA Kanda ya Serengeti
>>Mfanyabiashara wa Tanzania Nyambari Nyangwine sasa kuwekeza Uganda
>>Kamati ya Rufani Tarime yarejesha wagombea 100, CHADEMA, ACT Wazalendo waipongeza
>>Kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo: Rais Samia aagiza majengo yote yakaguliwe
No comments:
Post a Comment