
Dkt Stephen Kebwe
Na Mwandishi Maalumu/ Mara Online News
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Naibu Waziri wa Afya, Dkt Stephen Kebwe amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuwaletea Watanzania maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anafanya kazi nzuri sana kwenye miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu. Bajeti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo imekuwa ikiongezea kila mwaka,” Dkt Kebwe ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti kupitia chama tawala - CCM mwaka 2010 hadi 2015 alisema katika mahojiano maalum na Mara Online News kwa simu juzi.
Dkt Kebwe alimtabiria Rais Samia ushindi mnono kwenye uchaguzi mkuu ujao kutokana na kile alichokiita kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha, Dkt Kebwe alimpongeza Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa ushindi mkubwa ambao chama hicho kilipata katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, mwaka huu.
“Ushindi ambao CCM imepata kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni kiashiria tosha kuwa CCM itapata ushindi mnono katika uchaguzi mkuu jao,” alisema mwanasiasa huyo anayetajwa kuwa mpole lakini mwenye mikakati mizuri ya maendeleo.
Alipoulizwa kama bado ana nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Serengeti kupitia CCM mwakani, alijibu kwa kifupi “Niko barabara” bila kufafanua.
Mwaka 2020, Dkt Kebwe aliibuka mshindi wa kwanza wa kura za maoni ya ubunge ndani ya CCM katika jimbo la Serengeti lakini vikao vya chama hicho ngazi ya juu havikurudisha jina lake.
No comments:
Post a Comment