
Mojawapo ya majengo ya shule za sekondari mpya zinazotarajiwa kufunguliwa Januari 2025 Musoma Vijijini.
-----------------------------------
Viongozi na wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini katika mkoa wa Mara hawataki mzaha linapokuja suala la maendeleo ya elimu.
Msimamo wao huo ndio umewasukuma kuwa na kipaumbele cha ufunguzi wa shule sita za sekondari mpya mapema Januari mwakani.
Jimbo la Musoma Vijijini lina kata 21 zenye vijiji 68 na vitongoji 374. Hivi sasa jimbo hilo linajivunia shule za sekondari za kata 26 na za binafsi mbili.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini, shule za sekondari zilizopangwa kufunguliwa mwakani ambazo zinajengwa kwa michango na nguvu za wananchi ni Rukuba Island, Nyasaungu na Muhoji.
Nyingine ni sekondari za Butata, Nyamrandirira (Ufundi) na David Massamba Memorial ambazo zinazojengwa kwa michango mikubwa kutoka serikalini na nguvu ya wanavijiji. Shule hizo kila moja imepokea shilingi milioni 584 kutoka serikalini.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alipata fursa ya kukagua majengo ya shule ya sekondari Muhoji, kata ya Bugwema itakayofunguliwa Januari 2025.

Prof Sospeter Muhongo
Taarifa ya ofisi ya Mbunge imeongeza kuwa vijiji sita vya Chitare, Kataryo, Kiriba, Mmahare, Musanja na Nyambono vimekubaliwa kuanza ujenzi wa sekondari mpya.
Pia, ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kwa kila sekondari ya kata unaendelea Musoma Vijijini.
Aidha, sekondari mbili za Suguti na Mugango za kidato cha tano na sita za masomo ya sayansi zinatarajiwa kuanzishwa katika jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment