NEWS

Tuesday, 3 December 2024

MVIWANYA wakutanisha wadau kujadili maendeleo ya kilimo mseto



Mratibu wa Mradi, Joel Nguvava akifafanua jambo katika mkutani huo. (Picha na Mara Online News)
--------------------------

Na Godfrey Marwa/ Mara Online News

MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Nyancha (MVIWANYA) umewakukutanisha wadau mbalimbali kujadili shughuli za kilimo mseto, ufugaji na mazingira zinazotekelezwa na mtandao huo kwa maendeleo ya jamii katika wilaya za Tarime, Rorya na Serengeti, mkoani Mara.

Miongoni mwa wadau hao, ni wajumbe wa Bodi ya MVIWANYA, wakulima na wafugaji, maafisa kilimo, mazingira na maendeleo ya jamii, pamoja na walimu wa shule za msingi na sekondari.

Mkutano huo ulifanyika mjini Tarime jana, ambapo wadau walijikita katika kutathmimi shughuli zilizotekelezwa na MVIWANYA kwa mwaka 2024, katika mradi wa ASILI B unaofadhiwa na Shirika la Vi Agroforestry.


Mratibu wa mradi huo, Joel Nguvava alifafanua kuwa lengo la mkutano huo ni kuangazia shughuli zilizofanyika vizuri na ambazo hazijafanyika vizuri ili kuweka mikakati ya maboresho ili kuifahamisha jamii kinachofanywa na kuhamasishwa na MVIWANYA.

Vile vile, jamii iweze kuongeza kipato kupitia wakulima na kuboresha maisha yao kupitia hifadhi ya mazingira, pamoja na urutubishaji wa ardhi.

"Wito wetu ni wakulima kuwa na mabadiliko chanya, hususan nyakati hizi za mabadiliko ya tabianchi, kujikita kwenye kilimo mseto ambacho kinakidhi tija na kuzalisha kulingana na mazingira.

“Pia, tunahamasisha wakulima kuungana na kuwa na sauti moja ili wawe na soko la uhakika na kuondokana na dhana ya kuuzia mazao shambani, wauze mazao yaliyoongezewa thamani," aliongeza Nguvava.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wilaya ya Serengeti, Bwenda Bayinga alielezea ushirikiano kama nyenzo mhimu inayochangia kuimarika kwa kilimo.

"MVIWANYA tumekuwa tukishirikiana kupanga mipango ya kilimo mseto Serengeti. Taasisi zingine unakwenda hawashirikishi watu wa ngazi ya wilaya wala maafisa ugani, matokeo yake uendelevu wa shughuli unakwama.

"Sekta ya kilimo imefanya kazi vizuri kwa sababu tumekuwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye amemshauri Mheshimiwa Rais vizuri na ndio maana kila afisa ugani ana pikipiki. Tuna kipimo cha kupimia afya ya udongo, mfano, Serengeti uzalishaji wa mahindi ni mkubwa," alisema Bayinga.

Nao wakulima walielezea tatizo la sumu kuvu kwenye mazao na kuiomba serikali kwa kushirikiana na mashirika kusaidia kuchukua hatua, ikiwemo kutoa elimu ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa.

"Hili ni tatizo kubwa lishughuliwe kwa kutoa elimu, litakuja kuathiri nguvu kazi ya Taifa, maana ukitupa mahindi yaliyoanza kuoza wengine wanachukua wanaenda kupikia gongo. Elimu itolewe wananchi wajue maana ya sumu kuvu na madhara yake," alisema mmoja wa wakulima.

Aidha, MVIWANYA walitoa zawadi mbalimbali, zikiwemo fedha taslimu, gamu buti, taa za sola, mifuko ya kinga kwa wakulima bora, jezi na mipira kwa shule na washindi bora wa uendelevu wa mazingira kutoka wilaya zote - Tarime, Rorya na Serengeti.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages