NEWS

Tuesday, 14 January 2025

Mnada wa Mifugo wa Kimataifa Magena wakwama kwa miaka zaidi ya 20

Ng'ombe

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Mnada wa Mifugo wa Kimataifa Magena uliopo wilaya ya Tarime inayopakana na nchi ya Kenya, umeendelea kukwama kufunguliwa kwa miaka zaidi ya 20 sasa, baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutangaza nia ya kuufungua.

Sababu kuu inayokwamisha kufunguliwa kwa mnada huo inatajwa kuwa ni kutotolewa kwa shilingi milioni 150 kutoka wizara yenye dhamana ya mifugo kwa ajili ya kugharimia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu muhimu.

Mnada huo ambao ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa wafugaji na wafanyabiashara ya mifugo, hauna ofisi na vyoo, miongoni mwa miundombinu mingine.

Wafugaji wengi wilayani Tarime, ambao ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mifugo katika Afrika Mashariki, baadhi yao wanalazimika kuichepusha kwenda kuiuza nje ya nchi kwa bei ya chini.

Kwa miaka zaidi ya 20 sasa, kufunguliwa kwa mnada huo kumeishia kuwa kivuli cha ahadi zisizotekelezwa, hali inayoathiri sekta ya mifugo na uchumi wa eneo hilo kwa ujumla.

Vile vile, kutofunguliwa kwa mnada huo kunaikosesha serikali mapato na kusababisha watu wengi kukosa ajira na fursa ya biashara ya kimataifa.

“Mnada huu ukifunguliwa utasaidia kuendeleza biashara ya mifugo, kuongeza mapato kwa wafugaji, wafanyabiashara na serikali, lakini pia kuchochea ukuaji wa uchumi wa wilaya ya Tarime,” alisema mkazi wa mtaa wa Magena, Justin Manga katika mazungumzo na Mara Online News hivi karibuni.

Juni 12, 2021, Waziri wa Maendeleo ya Mifungo na Uvuvi wa wakati huo, Mashimba Ndaki alifika Magena na kuiagiza Halmashauri ya Mji wa Tarime kutangaza siku rasmi ya mnada huo, ambapo baadaye ilitangazwa kuwa ni Alhamisi, na kwamba ungefunguliwa Julai 22, 2021.

Aidha, Ndaki aliiagiza halmashauri hiyo kutumia mapato ya ndani kugharimia matengenezo ya barabara zinazoelekea kwenye mnada huo wenye eneo lenye ukubwa wa ekari 100, ili kuwezesha magari makubwa kuingia.

Hata hivyo, akizungumza na Mara Online News kupitia simu ya kiganjani, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote alisema suala la kufunguliwa kwa mnada huo bado ni kitendawili kigumu.

“Labda serikali haijapata shilingi milioni 150 ilizoahidi kutoa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na vyoo vya mnada,” Komote alisema.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages