
Baadhi ya wanafunzi na walimu wa Shule mpya ya Msingi Kenyangi wilayani Tarime, na wafanyakazi wa Idara ya Mahusiano ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wakifurahia picha ya pamoja wakati wa mapokezi ya wanafunzi shuleni hapo jana Jumatatu. (Picha na Mara Online News)
----------------------------------------
SHULE ya Msingi mpya ya kisasa ya Kenyangi iliyojengwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika kijiji cha Matongo wilayani Tarime, imeanza kutumika rasmi baada maamia ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba kuripoti jana Jumatatu.
Shule hiyo imejengwa kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi zaidi ya 800 waliokuwa wanatumia majengo ambayo yanapisha upanuzi wa shughuli za mgodi huo.
Ujenzi wa shule hiyo umehusisha vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, jengo la utawala na vyoo vya kisasa.
Oktoba 6, 2024, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Dkt Mark Bristow alikabidhi shule hiyo ambayo ujenzi wake umegharimu mamilioni ya fedha kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals .
Akizungumza wakati wa mapokezi ya wanafunzi hao, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kenyangi, Hadija Nusura Sango aliushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kuwajengea shule ya kisasa yenye mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
"Hakika hii ni shule bora, wito wetu kwa wazazi ni kuwaleta watoto kupata elimu na kushirikiana na walimu kuwawezesha kutimiza ndoto zao," alisema Mwalimu Hadija.
Kwa upande wao, wanafunzi wa shule hiyo waliahidi kutendea haki miundombinu bora ya shule hiyo kwa kusoma kwa bidii na kuinua kiwango chao cha taaluma.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba Marwa aliushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kuendelea kuboresha mahusiano na jamii inayouzunguka kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Naye Meneja wa Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi aliwaomba walimu na wanafunzi kutumia na kutunza vizuri miundombinu na mazingira ya shule hiyo.
"Shule hii ni ya kwenu, sio ya mgodi, muitunze vizuri. Tunatarajia itakuwa na mazingira mazuri wakati wote, na inakuwa bora sio kimajengo pekee, bali pia kitaaluma," alisema Uhadi.
Aidha, aliahidi kuwa mgodi huo utaendelea kushirikiana na serikali kujenga miundombinu bora ya huduma za kijamii kila inapotwaa maeneo ya wananchi kwa ajili ya upanduzi wa shughuli za uchimbaji madini.
No comments:
Post a Comment