NEWS

Tuesday, 14 January 2025

Tarime Vijijini: Kiles amwaga misaada ya mamilioni kwa vikundi, vitongoji katani Nyakonga



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati) akikabidhi kwa vikundi pikipiki zilizotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Simion Kiles “K” (aliyeshikilia kipaza sauti) katani Nyakonga jana.
-----------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara, Simion Kiles "K" ametoa na kukabidhi misaada mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 17 kwa vikundi vitano na vitongoji 12 vilivyopo kata ya Nyakonga.

Misaada hiyo ni pikipiki mbili zenye thamani ya shilingi milioni 5.4 na viti zaidi ya 360 vyenye thamani ya shilingi milioni nane kwa vitongoji 12 kwa ajili ya shughuli za maafa.

Aidha, Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga, alivipatia vikundi vitatu vya wajane msaada wa shilingi milioni moja kila kikundi kwa ajili ya kujiinua kiuchumi.

Kiles alikabidhi misaada hiyo kwa vikundi hivyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Magoto katani Nyakonga, mbele ya viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.

"Na wengine muanzishe vikundi viwawezeshe kupata mikopo ya halmashauri na pia mpate misaada kama hii kutoka kwa wadau ili iwawezeshe kujiinua kiuchumi, maana hizi fedha siyo kwa ajili ya kula,” alisema Kiles.


Mwenyekiti Kiles (mwenye miwani) na DC Gowele (katikati) wakikabidhi sehemu ya msaada wa viti kwa kiongozi wa kitongoji katani Nyakonga jana. (Picha zote na Mara Online News)
-----------------------------------

Mwenyekiti huyo wa halmashauri alitumia nafasi hiyo pia kutuma wito kwa wadau wa maendeleo kumshirikisha pale wanapotoa misaada katika kata yake na kwamba hatashirikiana na wale wanaofanya kinyume.

Kwa upande wao viongozi wa vikundi vilivyonufaika na misaada hiyo walimshukuru Kiles wakisema vifaa hivyo vitawasaidia katika kujikwamua kiuchumi.

"Niseme kwamba ni jambo la heri na la kipekee kwa huu msaada wa leo kwa sababu utatusaidia namna ya kujiondoa katika wimbi la umaskini,” alisema Eliakim Samwel Mniko, Mwenyekiti wa Kikundi cha Green Guard.

Awali, Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele alihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Magoto na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Nyakonga.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages