NEWS

Tuesday, 14 January 2025

Tume ya Madini yatoa tahadhari ongezeko la matumizi ya baruti nchini



Baruti/ vilipuzi

Na Mwandishi Wetu

Tume ya Madini nchini imetoa tahadhari kuhusu ongezeko kubwa la matumizi ya baruti katika shughuli za uchimbaji madini, na kutaka uwepo udhibiti kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea siku za usoni.

Ilitoa tahadhari hiyo jijini Dodoma jana wakati wa kikao cha kuwajengea wakaguzi wa migodi na baruti uwezo, ambapo ilihimizwa kuwepo usimamizi madhubuti wa sheria, sera na kanuni ili kuepusha maafa yanayoweza kuletwa na ongezeko la matumiziya vilipuzi hivyo.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Mhandisi Ramadhani Lwamo, matumizi ya baruti nchini yameongezeka kutoka wastani wa tani 3,000 katika miaka ya 1990 hadi kufikia wastani wa tani 26,516.07 mwaka 2024.

Mhandisi Lwamo alisema ongezeko hilo limesababishwa pia na ongezeko la shughuli za uchimbaji wa madini, utafiti wa mafuta na gesi asilia na ujenzi wa miundombinu.

Hali kadhalika, ongezeko la matumizi ya baruti alisema pia limesababisha kushamiri na kupanuka kwa biashara ya vilipuzi hivyo.

Mhandisi Lwamo alisema mpaka sasa kuna bohari zaidi ya 231, stoo 493 na masanduku ya kuhifadhia baruti zaidi ya 279 yaliyosajiliwa kwa ajili ya kutunzia baruti migodini na maeneo ya biashara ya baruti.

“Matumizi makubwa ya baruti maana yake uchimbaji umeongezeka; hivyo bila udhibiti kutakuwepo madhara. Kikao hiki ni kujengeana uwezo, lengo likiwa kuhakikisha wachimbaji hawapotezi maisha au viungo kwa sababu ya matumizi ya baruti,” Mhandisi Lwamo alisema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini nchini, Hamisi Kamando alisema kumekuwepo na matukio mbalimbali ya ajali kwa sababu ya kutozingatiwa kwa Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963 na Kanuni za Baruti za Mwaka 1964.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages