NEWS

Friday, 10 January 2025

Tanzania, Uingereza kushirikiana kuwajengea wananchi uwezo sekta ya madini



Waziri wa Madini Tanzania, 
Anthony Mavunde.
----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Tanzania na Uingereza zimekubaliana kuendeleza sekta ya madini, hasa katika kuwajengea wananchi uwezo na kuongeza thamani katika mnyororo wa madini mkakati.

Ushirikiano wa nchi hizo, kwa mujibu wa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, utagusa maeneo ya mafunzo kwa Watanzania waliojiajiri katika sekta ya madini, kubadilishana uzoefu, kuwekeza kwenye tafiti mbalimbali ili kukuza sekta hiyo na kupanua mnyororo wa thamani.

Waziri Mavunde amesema lengo ni kuwavutia wawekezaji waweze kuzalisha ajira na kuchangia ukuaji wa pato la taifa.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam Jumatano wiki hii alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini, Marianne Young, ambaye alimtembelea ofisini kwake kujitambulisha.

Chini ya ushirikiano huo, kutakuwa na kubadilishana uzoefu baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini ya Tanzania (GST) na Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya Uingereza (BGS) ili kuwajengea Watanzania uwezo.

Mavunde alisema Uingereza imeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika kuongeza thamani kwa madini ya mkakati kwa kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya madini mkakati.

“Sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha kwamba madini ya kimkakati yanawanufaisha Watanzania na taifa. Tumeandaa mkakati maalum wa kutekeleza azma hiyo, ikizingatiwa kuwa madini hayo sasa yana mahitaji makubwa duniani,” alisema Mavunde.

Aliongeza: “Tupo hatua ya mwisho ya kukamilisha mkakati huu maalum wa madini mkakati ambao pia ni sehemu ya kampeni ya dunia katika kupunguza hewa ya ukaa kupitia nishati safi.”

Naye Balozi wa Uinjgereza, Marianne, aliipongeza Tanzania kwa kipaumbele cha ukuaji wa sekta ya madini, akiahidi ushirikiano kuhakikisha madini mkakati yanaongezewa thamani.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages