NEWS

Thursday, 16 January 2025

Tarime: DC Gowele aingilia kati mgogoro wa ardhi uliokwamisha ujenzi wa sekondari katani Nkende



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele akihutubia mkutano wa hadhara katani Nkende jana Januari 16, 2025.
---------------------------------------

Na Godfrey Marwa/ Mara Online News

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele ameingilia kati mgogoro wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 25, uliodumu kwa miaka miwili na kukwamisha ujenzi wa shule ya sekondari katika mtaa wa Romori, katani Nkende.

Meja Gowele alifika na kuzungumza na wananchi katani hapo jana Januari 16, 2025 baada ya kupata malalamiko kwamba familia mbili zimeendelea kutumia ardhi hiyo inayoelezwa kutengwa kwa ajili ya shughuli za umma.

Kiongozi huyo aliitaka Halmashauri ya Mji wa Tarime kutambua na kulinda maeneo ya umma, ili yaweze kutumika kujengwa miradi ya maendeleo ya wananchi kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

"Halmashauri ya Mji endeleeni kutambua maeneo yote ya umma, yalindwe na yasivamiwe, bado tuna mahitaji makubwa ya maeneo ya miradi mikubwa ya maendeleo," alisema Meja Gowele.

Aliendelea: “Tumepata mradi mkubwa wa ujenzi wa shule ya sekondari. Nimetoa nafasi kwa wanaoendelea kulima kwenye eneo lile kuleta nyaraka za uthibitisho ili tutende haki, kama hawana, Halmashauri mwendelee na utaratibu wa ujenzi wa shule ambayo itahudumia watoto wetu.”


Wananchi wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya katika mkutano huo wa hadhara.(Picha zote na Mara Online News)
-------------------------------------

Mwenyekiti wa Mtaa wa Romori, Zacharia Mwita Chacha alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufika mtaani hapo kusikiliza wananchi na kuelekeza utatuzi wa kero hiyo.

"Kero hii ilikuwa changamoto kwa wenyeviti wa mitaa mitatu - hatulali, ukikaa kidogo unasikia mwananchi anauliza tumefikia wapi kuhusu mkakati wetu wa shule,” alisema Chacha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime na Diwani wa Kata ya Nkende, Daniel Komote aliwaomba wananchi hao kuwa na utayari wa kushirikiana na serikali katika jitihada za kuwaletea maendeleo ya kijamii, ukiwemo ujenzi wa shule hiyo.

“Serikali imeonesha nia ya dhati kwa kuleta fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kusoma na kutimiza ndoto zake,” alisema Komote.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages