
Freeman Mbowe
Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe amewashangaa watu wanaomtaka ang’atuke eti kwa sababu tu amekaa madarakani kwa miaka 20.
Mbowe amekataa kuachia madaraka akisema anahitaji muhula wa mwisho (miaka mitano zaidi) ili aweze kutimiza ndoto yake katika chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania.
“Ninajivunia kujenga chama kikuu cha upinzani na chenye mtandao nchi nzima… miaka hii yote nimejenga na wenzangu chama kikubwa cha siasa nchini,” Mbowe alisema katika mahojiano maalum na BBC jana Jumatatu.
Akisisitiza msimamo wake, Mbowe alisema: “Siwezi kukimbia kuondoka [madarakani] wakati hatujakamilisha ndoto. Binadamu tunafanya kazi kwa malengo, na malengo ni ndoto.”
Aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa bado ana uwezo wa kukiongoza CHADEMA, na kwamba yeye siyo kiongozi pekee aliyedumu madarakani muda mrefu.
“Hata huyu mgombea mwenzangu Mheshimiwa Lissu amekaa Kamati Kuu [ya CHADEMA] miaka 20. Siyo kweli kwamba kila damu changa ina uwezo kuliko damu ya zamani, hiyo ni dhana potofu, ni udhalilishaji vilevile,” alisema Mbowe ambaye mwaka huu anachuana na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), Tundu Lissu katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa kitaifa wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment