NEWS

Sunday, 16 February 2025

Bunda: Taasisi ya Ryakitimbo ilivyochangia maendeleo ya wananchi Chamuriho



Mwenyekiti wa Ryakitimbo Foundation, Moses Wambura Ryakitimbo akiwa katika maktaba ya vitabu vya kusoma.
----------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu/ Mara Online News

Huwezi kuzungumzia maendeleo ya wilaya ya Bunda, hususan katika tarafa ya Chamuriho bila kutaja jina la Ryakitimbo Foundation. Hii ni kutokana na jinsi taasisi hiyo ilivyoigusa jamii katika sekta ya elimu, afya, umeme, ujasiriamali, kilimo na michezo.

Taasisi hiyo ambayo inafanya kazi chini ya Mwenyekiti wake, Moses Wambura Ryakitimbo, ilisajiliwa kwa lengo la kuenzi shughuli za maendeleo zilizokuwa zikifanywa na Mzee John Magige Ryakitimbo (kwa sasa ni marehemu).

Akiwa Mwenyekiti wa Ikizu Development Association (IDA), mzee huyo alifanikisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Makongoro katika miaka ya 1980 na ujenzi wa msingi wa Shule ya Sekondari Hunyari, miongoni mwa mambo mengine mengi ya maendeleo katika huduma za jamii.

Katika kipindi cha mwaka 2022-2025, Ryakitimbo Foundation imeweza kujitolea kufanikisha mambo mengi ya maendeleo ya wananchi ndani na nje ya tarafa ya Chamuriho, wilayani Bunda.

Mfano, imekuwa ikiweka umeme katika shule ambazo hazina umeme ili kuwasaidia wanafunzi kujisomea wakati wa usiku, na hata kuwezesha matumizi ya kompyuta.

“Pia, tumeweza kugawa misaada ya madawati, photocopy machines, madaftari na kuchangia vifaa vya ujenzi katika shule na zahanati,” Mwenyekiti wa Ryakitimbo Foundation, Moses Wambura Ryakitimbo aliiambia Mara Online News wilayani Bunda wiki iliyopita.

Wambura anataja misaada mingine iliyotolewa na taasisi hiyo kuwa ni vifaa tiba, mbegu kwenye kaya masikini na kuendesha semina za mafunzo ya ujasiliamali na kilimo.

Aidha, imejenga mabanda ya bodaboda ili kuwasaidia vijana kujikinga dhidi ya mvua na jua kali. “Ujenzi wa mabanda haya unaendana na semina za usalama barabarani,” anasema Wambura.

Lakini pia, Ryakitimbo Foundation inatoa fedha taslimu kusaidia vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali, kwa mujibu wa mwenyekiti huyo.

Kuhusu michezo, taasisi hiyo imekuwa ikiandaa mashindano ya bao ili kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kusemea kwa wananchi maendeleo makubwa yanayofanywa na Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.


Sehemu ya wachezaji wanaoshiriki mashindano ya michezo yanayoandaliwa na Ryakitimbo Foundation.
--------------------------------------

“Mashindano ya bao yalifanyika sambamba na kununua sare za kikundi cha ngoma za asili ya Ekhesa na Bwenga, tukiamini kwamba ngoma hiyo inapaswa kuenziwa kwa vizazi vingi vijavyo anasema Wambura.

Anaongeza: “Pia, tunaendesha mashindano ya soka kila mwaka kwa watoto, wanawake na vijana, ambapo mshindi wa kwanza hupokea zawadi ya shilingi milioni mbili ambazo tunaamini zitawasaidia vijana kujiajiri.”

Hawakuishia hapo, kwani pia walifanikiwa kumleta nguli wa soka Tanzania, mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Edibily Lunyamila kuendesha semina za michezo hiyo kwa vijana ili kuwasaidia kufika mbali, ambapo alichukua baadhi ya vijana kwa ajili ya majaribio katika timu za Yanga na Pamba.

Vile vile, Ryakitimbo Foundation inadhamini timu ya Chamuriho FC ambao ni mabingwa wa soka Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Bunda mwaka 2024, na imepandishwa kucheza Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Mara.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Ryakitimbo Foundation, Moses Wambura Ryakitimbo aliweza kuchangisha taasisi hiyo na wadau wake shilingi millioni 12 katika tamasha la harambee ya ujenzi wa Kituo cha Utamaduni wa Ikizu, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, DkT Vicent Anney.

Bado Ryakitimbo Foundation ina mipango mingi, ikiwemo kushawishi mamlaka husika kuunganisha vivutio vilivyopo katika tarafa ya Chamuriho na utalii wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Mipango mingine Wambura anasema ni kugawa misaada ya bima za afya kwa familia zisizokuwa na uwezo, ujenzi wa visima, maktaba ya vitabu vya kujisomea, maabara za kompyuta na masomo ya sayansi.

“Pia, taasisi yetu kwa kushirikiana na wadau wake ipo katika mchakato wa uundaji wa Chamuriho Community Saccos Kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupata mikopo isiyoumiza, ili waweze kujiajiri na kuzalisha, na hivyo kukidhi mahitaji ya familia zao.

“Ryakitimbo Foundation inaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo ya Serikali chini ya Rais Dkt Samia, bila kusahau michango mbalimbali tunayopeleka katika taasisi za dini na chama,” anaongeza Wambura.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages