
Msaada wa vitabu kutoka Nyambari Nyangwine Foundation ukikabidhiwa katika Shule ya Sekondari Bukenye katani Manga jana Februari 14, 2025.
------------------------------------
Hatimaye kata za Manga, Kibasuka na Kiore zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) nazo zimefikiwa na msaada wa vitabu vya shule za sekondari kutoka Taasisi ya Nyambari Nyangwine (NNF).
Sekondari nne; ambazo ni Bukenye, Kibasuka, Kewamamba na Nkerege zilizopo katika kata hizo zilikabidhiwa msaada wa vitabu vya kiada na ziada jana Februari 14, 2025 na mwakilishi wa taasisi hiyo, Sospeter Migera Paul.
Mwishoni mwaka jana, Nyambari Nyangwine aliipatia Shule ya Sekondari Manga msaada wa vitabu vya O-Level na A-Level.

Makabidhiano ya msaada wa vitabu katika Sekondari ya Manga mwishoni mwa mwaka jana.
-------------------------------------

Makabidhiano ya msaada wa vitabu
katika Sekondari ya Nkerege jana.
------------------------------------
Walimu na wanafunzi wa shule hizo waliishukuru taasisi hiyo wakisema vitabu hivyo vitarahisisha ufundishaji na kuwaongezea wanafunzi ari ya kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao za elimu.

Makabidhiano ya msaada wa vitabu
katika Sekondari ya Kewamamba jana.
------------------------------------
Viongozi na wananchi walioshiriki katika hafla za makabidhiano ya msaada huo wa vitabu nao walishukuru na kuwahimiza wanafunzi kukazania masomo ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.
"Tunamshukuru Nyambari Nyangwine, nilimuomba vitabu na ameleta hapa Bukenye Sekondari, vitendea kazi pamoja na vitabu vinapokuwa vimekosa shule haitafanya vizuri. Tunataka awamu inayokuja tupate matokeo mazuri," alisema Steven Gibayi Chacha, Diwani wa Kata ya Manga.

Makabidhiano ya msaada wa vitabu
katika Sekondari ya Kibasuka jana.
------------------------------------
Naye mkazi wa kata ya Kibasuka, Matiko Nyaiho alisema: "Tunaona Nyambari Nyangwine anavyopenda wanafunzi na watu wa Kibasuka, ukiona mtu amekuletea vitabu kama hivi ujue anataka watu wawe na mwanga wa elimu - tupate wanasayansi, wanamahesabu ili watusaidie kuendesha nchi.”

Mkazi wa Kibasuka, Matiko Nyaiho
(aliyevaa kofia) akizungumza jana.
-----------------------------------
Msaada wa vitabu kwa shule za sekondari unaotolewa na Nyambari Nyangwine Foundation ni sehemu ya kuunga juhudi za serikali za uwekezaji na uboreshaji wa elimu nchini kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata vifaa muhimu vya kujifunzia ili waweze kufikia ndoto zao za elimu.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>HABARI PICHA:Rais Samia ashiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika
>>Tarime: Heche kuchinja ng’ombe 20 kujipongeza kwa ushindi CHADEMA
>>Mwanafunzi wa sekondari afa kwa kugongwa na basi la Kisire Tarime
>>Hali za MNEC Gachuma, DC Kemirembe zaimarika, waruhusiwa hospitalini Bugando
No comments:
Post a Comment