NEWS

Thursday, 20 February 2025

CCM yakemea mbinu chafu za ‘kupita bila kupingwa’ katika uchaguzi



Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitawakubali wagombea wake wa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi watakaotumia mbinu chafu za kutaka kupita bila kupingwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu

“Chama hakitasita kuwaengua wale watakaokiuka katiba, kanuni na maadili ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025,” Katibu Mkuu wa Chama hicho tawala, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi ameonya.

Amesema tayari baadhi ya wanachama wameanzisha kampeni kwa kutumia mbinu za kuanzisha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, au kufadhili matukio ya kijamii kama vile harusi, misiba, siku za kuzaliwa na kushinikiza ili wapitishwe bila kupingwa.

“Tunawataka waache mara moja. CCM ina mfumo madhubuti wa kufuatilia mwenendo wa wanachama wake, na kumbukumbu hizi zinahifadhiwa. Wanaweza kushangaa majina yao yakiwekwa pembeni,” ametahadharisha.

Dkt Nchimbi aliyasema hayo jana jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makatibu wa matawi na kata wa wilaya ya Dodoma.

Kwa madiwani na wabunge walioko madarakani, aliwataka kuacha kupuuza majukumu yao kwa kisingizio cha maandalizi ya uchaguzi.

Alisema CCM itafanya tathmini ya kila mgombea kulingana na utendaji wake na wala si kwa uwezo wake wa kutoa fedha kwa wapiga kura.

“Tumeshuhudia watu wakichaguliwa lakini wanakaa miaka mitano bila kufanya kazi kwa sababu wanajua wapiga kura wachache ndani ya chama watawarudisha tena madarakani,” alisema Dkt Nchimbi.

Aliongeza: “Mfumo wetu mpya unalenga kumchagua mgombea kwa misingi ya kazi zake wala si kwa kutumia rushwa, au mbinu za kificho. Tunataka ukichaguliwa ufanye kazi kwa wananmchi.”

Dkt Nchimbi alisema CCM kimebaini matukio ya kifisadi ya baadhi ya wabunge na madiwani wakipitisha fomu ili watangazwe kuwa wamepita bila kupingwa, jambo ambalo ni kukiuka taratibu za chama hicho.

Alisema wapo wanachama wanaoandaa kumbukumbu za misiba, siku za kuzaliwa na hata sherehe za arusi na kuwapa posho wahudhuriaji waliovaa sare za CCM ili ionekane kwamba ni mkutano wa kisiasa.

Alisisitiza kwamba CCM sasa imekuja na tiba ya kufuatilia nyendo za wanachama laghai wanaotaka kupata uongozi kwa hila na kuwaengua.

Alisema wanachama wote walioanzisha mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwa malengo ya kisiasa, wale wanaotumia mbinu chafu za kuwapaka matope viongozi waliokuwa madarakani, nafasi yao ya kupenya kugombea nafasi wanazowania itakuwa ni finyu kwani watapigwa ‘panga’.

Katika miaka ya karibuni, wapiga kura wa Tanzania wameshuhudia kushamiri kwa vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi na upotoshaji wa dhana ya uongozi kwamba lazima uwe na uwezo wa kuhonga.

Rushwa imejipenyeza zaidi baada ya kuparaganyika kwa mfumo wa udhibiti, hivyo kutoa mwanya kwa wenye pesa kuvuruga taratibu za kuchuja wagombea kwa kuzingatia uadilifu wao na uzalendo kwa taifa lao.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages