
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Sadiki Nombo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mjini Musoma jana Alhamisi.
------------------------------
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imebaini dosari mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ya kijamii ipatayo 10 yenye thamani ya shilingi 7,947,792,718.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TAKUKURU Mkoa wa Mara, miradi hiyo ni miongoni mwa miradi 43 yenye thamani ya shilingi 16,501,356,057 ya sekta za afya, elimu, barabara na maji iliyofuatiliwa na taasisi hiyo mkoani humo katika kipindi cha Oktoba - Desemba 2024.
“Miradi hii imefuatiliwa kwa kufanyiwa ukaguzi ili kujua ubora na thamani ya fedha iliyotumika,” Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Sadiki Nombo aliwambia waandishi wa habari mjini Musoma jana Alhamisi.
Kwa upande mwingine, TAKUKURU imefanikiwa kunusuru mifuko 1,473 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 37 kwenye mradi wa Chuo cha VETA Burunga, wilayani Serengeti.
“Katika ufuatiliaji tulibaini manunuzi makubwa ya saruji katika awamu ya kwanza ya mradi huo wenye thamani ya shilingi 1,483,532,660 yaliyopelekea mifuko 1,473 ya saruji kubaki stoo ilihali ujenzi umekamilika,” alisema Nombo.
Baada ya kubaini dosari, TAKUKURU ilimshauri msimamizi wa mradi huo ambaye ni Mthibiti Ubora wa Shule Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuomba kibali cha matumizi ya saruji hiyo kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambapo kibali kilitolewa ikatumika kwenye hatua nyingine ya utekelezaji wa mradi.
No comments:
Post a Comment