
Dkt Vincent Naano Anney
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amewabadilishia wakuu wa wilaya wawili vituo vya kazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam jana Februari 21, 2025, Rais Samia amemhamisha Mkuu wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Dkt Vincent Naano Anney kwenda wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Vile vile, Rais Samia amemhamisha Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Enock Kaminyonge kwenda wilaya ya Bunda.
Wakati huo huo, Rais Samia amemteua CPA Juma Ajuang Kimori kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO), nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Yona Killagane aliyemaliza muda wake.
Prof Edward Gamaya Hoseah ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, akichukua nafasi ya Deo Mtasiwa aliyemaliza muda wake.
Renatha Mtunda Rugarabamu ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), akichukua nafasi ya Emmanuel Humba aliyemaliza muda wake.
Jaji Mstaafu Awadh Mohammed Bawazir amteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), kuchukua nafasi ya Jaji Mstaafu Sauda Mjasiri aliyemaliza muda wake.
Naye Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa kwa kipindi cha pili.
No comments:
Post a Comment