NEWS

Friday, 28 February 2025

Trump na Zelensky wazozana Ikulu ya White House, mkutano wavunjika, aondoka kwa hasira




Mkutano wa pamoja na wanahabari umeahirishwa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump (pichani kulia) kumwambia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky (kushoto) "amemkosea heshima" na kusema "tufanye makubaliano au tuondoke".

Rais Zelensky ameondoka Ikulu ya Marekani ya White House baada ya majibizano makali na Rais Trump na Makamu wake, JD Vance.

Baada ya tukio hilo lililooneshwa moja kwa moja kutoka White House, Rais wa Ukraine anaonekana akitoka ofisini na kuingia kwenye gari jeusi aina ya SUV, ambalo liliondoka kwa kwa haraka.

Muda mfupi baadaye, Trump alichapisha ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social akidai kwamba Zelensky "aliidharau Marekani katika Ofisi yake ya Oval inayopendwa. Anaweza kurejea akiwa tayari kwa mazungumzo ya amani."

Huku hayo yakijiri, Ikulu ya White House imesema Trump na Makamu wake, JD Vance "hawatakubali watu wa kutumiwa vibaya".

Katika taarifa iliyotolewa muda mfupi baada ya mkutano wao na Zelensky, Ikulu ya White House imesema wawili hao "daima watazingatia maslahi ya Wamarekani na wale wanaoheshimu nafasi ya Marekani duniani".

Moja ya maneno waliyorushiana Trump na Zelensky katika Ikulu ya Marekani, ni kwamba kiongozi huyo wa Ukraine anacheza na vita ya tatu ya dunia. Trump alisema “Unacheza na vita ya tatu ya dunia”.

Alisema hivyo baada ya Rais Zelensky kuonekana kutounga mkono mazungumzo ya Rais Trump na makamu wake, JD Vance kuhusu namna Ukraine inavyoshughulika na mzozo wake na Urusi.

Kwa upande wake Zelensky alimwambia Trump “usimchekee muuaji”, akimrejea Rais wa Urusi, Vladmir Putin. Marekani inataka Ukraine ikubaliane na Urusi kumaliza mzozo huo kwa namna ambayo Zelensky hakubaliani nayo.

Awali, kwa mujibu wa mshirika wetu wa Marekani, CBS, wawakilishi wa Ukraine waliondoka kutoka Ikulu ya Marekani kupitia “chumba kilichotengwa.” Mshauri wa Usalama wa Taifa, Mike Waltz na Waziri wa Nje, Marco Rubio, waliwambia waondoke katika Ikulu ya White House.

Mkutano uliopangwa wa waandishi wa habari ambapo Zelensky na Trump wangezungumza kwa pamoja ulifutwa muda mfupi baada ya mzozo wa marais hao katika Ikulu ya White House.

Katika ziara yake hiyo nchini Marekani jana Ijumaa, Rais Zelensky alitarajiwa kusaini makubaliano yatakayoipa Marekani sehemu ya rasilimali adimu za madini za Ukraine.

Chanzo: BBC
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages