NEWS

Saturday, 1 March 2025

Tarime Mjini: Nyamisangura FC yatwaa ubingwa Matiko Cup 2024/2025



Mdhamini mkuu wa Matiko Cup 2024/2025, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Matiko akizungumza kwenye uwanja wa Serengeti jana.
------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Timu ya Nyamisangura FC imetwaa ubingwa wa mashindano ya soka ya Matiko Cup 2024/2025, katika fainali iliyochezwa jana Februari 28, 2025 kwenye uwanja wa Serengeti “Shamba la Bibi” mjini Tarime, Mara.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali, Nyamisangura iliishinda timu ya Giants FC ambayo imeshika nafasi ya pili, huku timu ya Watumishi wa Tarime Mji "HAMTA" ikishika nafasi ya tatu baada ya kuifunga timu ya Tarime United.




Zawadi kwa washindi wote wa mashindano hayo zitatolewa kesho Machi 2, 2025 uwanjani hapo, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Dkt Doto Biteko.

"Mshindi wa kwanza tutampa kombe na shilingi milioni 15, wa pili milioni 10, wa tatu milioni tano, wa nne milioni mbili na timu zote shiriki kila moja itapokea shilingi laki tano," mdhamini mkuu wa Matiko Cup 2024/2025, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Esther Matiko alisema.

Mbunge huyo alisema mashindano hayo yameitangaza zaidi wilaya ya Tarime na kuvutia wawekezaji wengi.

"Michezo hii imeitangaza zaidi Tarime, hapa meseji ni nyingi, pongezi ni nyingi na wadau ni wengi wanataka kuja Tarime na kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kuwekeza," alisema.




Kwa upande wake mgeni rasmi wa jana Ijumaa, Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye "Namba Tatu" alimpongeza Esther Matiko kwa kuanzisha mashindano hayo bila kujali itikadi za kisiasa.

Mbali na mchezo wa mpira wa miguu, mashindano ya Matiko Cup msimu wa 2024/2025 yalihusisha pia michezo mingine kama vile pool, bao na drafti, miongoni mwa mingine.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages