NEWS

Thursday, 27 March 2025

Rais Samia atoa milioni 100/- kusaidia waathirika wa maafa ya mvua Musoma Mjini



Mshauri wa Rais wa Mambo ya Siasa, Haji Omar Kheir (kushoto), akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati), msaada shilingi milioni 100 uliotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya waarhirika wa maafa ya mvua mjini Musoma jana. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Patrick Chandi Marwa.
-----------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Rais Samia Suluhu Hassan jana alitoa shilingi milioni 100 kuwasaidia wakazi wa mji wa Musoma walioathiriwa na maafa ya mvua kubwa iliyonyesha usiku wa Jumapili iliyopita.

Mvua hiyo ambayo iliambatana na upepo mkali iliezua paa za majengo ya makazi ya watu, biashara na taasisi mbalimbali, zikiwemo shule za msingi, kituo cha polisi, msikiti na kuharibu baadhi ya miundombinu ya umeme na barabara.

Mamia ya kaya yameripotiwa kuathiriwa na maafa hayo, huku watu wanane wakijeruhiwa.

Mshauri wa Rais wa Mambo ya Siasa, Haji Omar Kheir alikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kwa ajili ya kuwasaidia waathirika hao.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia, Kheir aliwashukuru waathiriwa wa maafa hayo kwa uvumilivu wao na kuwaahidi kwamba serikali yao itatatua changamoto zao bila kusita.

Alisema Rais Samia ameshawatuma washauri wake wa mambo ya siasa ili kutathmini hali halisi ya athari zilizosababishwa na mvua ili kujua mahitaji ya msaada.

Washauri hao wa Rais, ambao ni Haji Omar Kheir, Abdallah Bulembo na Balozi Rajab Omar Luhwavi, walitoa shilingi milioni 3.5 kuwasaidia waathirika waliopewa hifadhi katika kambi maalum mjini Musoma.


Viongozi wakitembelea familia zilizoathirika.
--------------------------------------

Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, ametoa mitungi mikubwa miwili ya gesi na majiko yake kwa ajili ya kupikia, huku Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete, akitoa kilo 100 za mchele.

Mkuu wa Mkoa, Kanali Mtambi, alisema wananchi wa Musoma wanamshukuru Rais Samia kwa ukarimu na upendo aliowaonesha tangu wakumbwe na maafa hayo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, naye alimshukuru Rais Samia kwa kuwafariji waathirika maafa hayo akisema ni ishara ya upendo wa dhati kwa wananchi.

Chandi aliwataka wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Rais Samia na viongozi wa mkoa huo katika kuwasaidia waathirika ili warejee katika maisha yao ya kawaida.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages