NEWS

Friday, 7 March 2025

Kamati ya Bunge ya Bajeti yazuru Mgodi wa Barrick North Mara, yaumiminia pongezi



Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti, Josephat Kandege (wa pili kutoka kulia mbele), Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (kulia mbele), wajumbe wa kamati hiyo na viongozi mbalimbali wakitembelea mgodi huo wilayani Tarime leo. (Picha na Mara Online News)
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti leo Machi 7, 2025 imetembelea Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wilayani Tarime kupata taarifa za maendeleo na kujionea shughuli za mgodi huo.

Mara tu baada ya kuwasili ilipata taarifa ya shughuli na maendeleo ya mgodi huo kutoka kwa Meneja Mkuu (GM), Apolinary Lyambiko kabla ya kutembelea kinu cha kuchenjua dhahabu (processing plant).

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Josephat Kandege, amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwao kwani imeiwezesha kujua mgodi unavyofanya kazi na namna unavyoshirikiana na jamii katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Tumepata fursa ya kujua mgodi unavyofanya kazi na unavyoshirikiana na jamii kutatua changamoto nyingi. Mfano uboreshaji wa huduma ya maji katika vijiji vinne tayari vinapata maji safi ya kunywa,” amesema Kandege ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kalambo mkoani Rukwa.

Kandege akizungumza katika ziara hiyo

Kandege pia ameeleza kufurahishwa na uwepo wa wafanyakazi wengi Watanzania katika mgodi huo, akiwemo Meneja Mkuu.

Wajumbe wa kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pia wamepongeza kampuni ya Barrick kwa kuendelea kuzingatia sheria za nchi, ikiwemo za kodi na hivyo kuwa na mchango mkubwa wa mapato kwa taifa.

Wabunge hao pia wameonesha kufurahishwa na kiasi kikibwa cha fedha kinachotolewa na kampuni ya Barick kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

“Takwimu zinaonesha Barrick North Mara inatumia sio chini ya shilingi bilioni saba kwenye miradi ya CSR kila mwaka, kwa kweli ni pesa nyingi na inagusa sana jamii,” amesema Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.

Naye Mbunge wa Viti Maalum ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Stella Ikupa Alex ameipongeza Barrick kwa kuendelea kufanya vizuri kisekta, huku akitolea mfano wa tuzo mbalimbali ambazo imetunukiwa, ikiwemo ya mwajiri bora nchini.

“Tuzo hizi ni nyingi, nami niwapongeze Barrick na CSR yenu inaonekana kwa ukubwa sana,” amesema mbunge huyo.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo akizungumza

Pia, Mbunge wa Jimbo la Meatu, Leah Komanya ameupongeza mgodi huo kwa kutumia takriban shilingi bilioni moja kujenga Kituo cha Afya Genkuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

“Ujenzi wa Kituo cha Afya Genkuru ambao umefanywa na mgodi ni jambo zuru sana, niwapongeze pia kwa kutunza mazingira na kutengeneza ajira kwa vijana,” amesema Komanya.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ole, Juma Hamad Omar ameipongeza Barrick kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu katika mpango wake wa CSR, huku pia akieleza kuridhishwa na uwasilishaji uliofanywa na GM Lyambiko mbele ya kamati hiyo.

Awali, Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinaly Lyambiko, amesema mgodi huo umetumia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 15 kwenye miradi ya maendeleo ya jamii kupitia CSR.

GM Apolinary Lyambiko akizungumza.

Mbali na CSR, Barrick inalipa kodi mbalimbali, zikiwemo ushuru wa huduma (service levy) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mirabaha kwa vijiji vitano vinavyozunguka mgodi huo.

Lakini pia, GM Lyambiko amesema kampuni ya Barrick imefanikiwa kuhuisha maisha ya mgodi huo hadi mwaka 2040.

“Kuna mabadiliko makubwa yametokea na maisha ya mgodi sasa yatakuwa hadi mwaka 2040 badada ya mwaka 2028,” GM Lyambiko amesema.

Alisema kazi ya kuhuisha kwa kurefusha maisha ya mgodi wa North Mara inafanyika pia katika mgodi wa Bulynhulu uliopo wilayani Kahama, Shinyanga.

“Bado tunaendelea kufanya tafiti ili kuendeleza maisha ya mgodi na utafiti pia unaedelea katika mgodi wa Bulyanhulu ili kuongeza maisha ya mgodi wake,” amesema Lyambiko.

GM Lyambiko pia amesema uwekezaji mkubwa umefanyika kwenye suala la mazingira tangu mwaka 2019 ambao kampuni ya Barrick ilikuchukua hatamu ya kuendesha mgodi huo.

Pamoja na mambo mengine, kwenye suala la ‘local content’ asilimia 96 ya wafanyakazi wanaofanya wa mgodi huo ni Watanzania, kwa mujibu wa GM Lyambiko.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages