
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Edward Range, akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Maji mjini Musoma jana.
-----------------------------------
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) mkoani Mara, imefanikiwa kuvuka lengo la Ilani ya CCM la kufikia asilimia 95 ya wananchi wanaopata majisafi mijini kufikia 2025, ambapo kwa sasa imefikia asilimia 98 ya wanaopata huduma hiyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Akizungumza katika maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Maji mjini Musoma jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Edward Range, alibainisha kuwa idadi ya watu wanaonufaika na huduma hiyo katika manispaa hiyo kwa sasa ni 173,148.
Range alisema mamlaka hiyo pia inasambaza huduma majisafi kwa watu 21,568 sawa na asilimia 84.5 ya wakazi wa mji wa Shirati wilayani Rorya, na kwa watu 41,640 sawa na asilimia 70 ya wakazi wa mji wa Mugumu wilayani Serengeti.
Pia, inasambaza huduma hiyo kwa watu 69,981 sawa na asilimia 52.6 ya wakazi wa mji wa Tarime, watu 47,673 sawa na asilimia 34.1 ya wakazi wa Musoma DC, na watu 46,873 sawa na asilimia 28.8 ya wakazi wa Butiama DC.
Hata hivyo, alisema bei elekezi ya maji iliyopitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ni ya chini ambayo inaweza kusababisha MUWASA kushindwa kukidhi gharama za kujiendesha na kusambaza huduma ya maji kwa baadhi ya wananchi.
Range aliweka wazi kuwa MUWASA inajitegemea kwa asilimia 100 katika uendeshaji wa shughuli zake.
"Mgeni rasmi, mapato ya MUWASA ni wastani wa shilingi milioni 460 kwa mwezi ukilinganisha na gharama za uendeshaji ambazo ni wastani wa shilingi milioni 615 kwa mwezi - sawa na upungufu wa shilingi milioni 155 kwa mwezi," alisema.

Sehemu ya wadau wa maji wakifuatilia mada katika maadhimisho hayo.
------------------------------------
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na Mhasibu wa MUWASA, CPA Etropia Ndowo, alisema bei iliyopitishwa na EWURA haikidhi gharama za uendeshaji wa mamlala hiyo.
Tayari MUWASA imewasilisha andiko la kuiomba EWURA ipitishe bei mpya ya maji ili mamkala hiyo iwe na uwezo wa kifedha wa kuendelea kujiendesha.

Mkurugenzi wa Fedha na Mhasibu wa MUWASA, CPA Etropia Ndowo.
-------------------------------------
Naye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, alisema serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi na kwamba katika mkoa wa Mara jitihada za serikali na wadau mbalimbali zimerahisisha huduma ya maji kuwafikia wananchi wengi zaidi.
MUWASA ilitumia fursa ya maadhimisho hayo ya kilele cha Wiki ya Maji pia kutoa elimu kuhusu utendaji kazi wake na changamoto zinazoikabili kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wenyeviti wa serikali za mitaa Manispaa ya Musoma, miongoni mwa wadau wengine.
Mamlaka hiyo imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Maji kuanzia Machi 16 hadi 22 kila mwaka kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa maji. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu wa 2025 inasema "Uhifadhi wa Uoto wa Asili kwa Uhakika wa Maji".
UNAWEZA PIA KUSOMA:
»Nyambari Nyangwine kufadhili semina ya washairi wa Tanzania ili kuboresha ufanisi wao
»Taasisi ya Mwanzo Mpya yawanoa wanawake Tarime, yampongeza Rais Samia
»Namibia yamuapisha Rais wake wa kwanza mwanamke, Rais Samia ampongeza
»Serengeti: Mwenyekiti UVCCM Mara aunga mkono Serikali kufanikisha upatikanaji wa lishe mashuleni
No comments:
Post a Comment